Pemba. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewasili katika Uwanja wa Gombani Chakechake mjini hapa, kuongoza sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi zinazofanyika leo Jumapili, Januari 12, 2025.
Pamoja na wananchi, baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo za Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964 ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na makamu wake, Dk Philip Mpango.
Wengine ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud na Hemed Suleiman Abdulla na marais wastaafu.
Pia sherehe za maadhimisho hayo zimehudhuriwa na viongozi wengine wa serikali wakiwemo mawaziri na watendaji wakuu wa taasisi, mashirika na mabalozi kutoka nchi mbalimbali.
Baada ya kuingia uwanjani hapo saa 8:40 mchana, Dk Mwinyi ambaye ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizo amepokewa kwa shangwe, nderemo na vifijo akiwa kwenye gari la wazi lililozunguka uwanja mzima.
Kisha akapokea salamu ya Rais na kupigwa mizinga 21 na baadaye atapokea maandamano ya wananchi.
Gwaride lenye gadi 10 za majeshi ya ulinzi na usalama litapita mbele ya Rais kwa mwendo wa pole na haraka na kutoa heshima kisha gwaride litasonga mbele na kutoa salamu ya utii.
Kisha utaimbwa wimbo wa taifa wa Zanzibar na wimbo maalumu wa ukombozi na kuwaenzi mashujaa na gwaride litatoka uwanjani.
Baada ya gwaride kutoka uwanjani Rais Mwinyi atatoa neno la shukrani na kuwasalimia wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo, kisha kuondoka uwanjani hapo na kufuatia viongozi wengine.