MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, George Mpole yuko hatua za mwisho ili kujiunga na Singida Black Stars kwa mkopo wa miezi sita, baada ya uongozi wa TP Lindanda kutoridhishwa na kiwango alichonacho tangu alipojiunga na kikosi hicho cha jijini Mwanza.
Taarifa kutoka ndani ya Pamba Jiji zilizonaswa na Mwanaspoti ni kwamba, Mpole ni miongoni mwa washambuliaji wanaotolewa kwa mkopo katika dirisha hili dogo la usajili linalofungwa keshokutwa Jumatano, sawa na Mghana Eric Okutu atakayejiunga na KenGold ya Mbeya.
“Baada ya kukamilisha usajili wa washambuliaji, Habib Kyombo na Mathew Tegisi Momanyi tumeona Mpole tumtoe kwa mkopo na Singida Black Stars imeonyesha nia ya kumhitaji, lengo ni kudumisha uhusiano uliopo baina yetu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza baada ya Pamba kupewa wachezaji, Habib Kyombo, Hamad Majimengi na Mohamed Kamara kwa mkopo ndipo viongozi wa Singida wakatumia fursa hiyo ya kumhitaji Mpole ambaye bado wanaamini katika kikosi hicho atafanya vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mpole hakuwa tayari kuzungumzia juu ya taarifa hizo, huku akiweka wazi hatambui chochote hadi sasa na kusisitiza ni mchezaji halali wa Pamba na bado ana mkataba uliobakia hivyo, hajui kuhusu kutolewa kwa mkopo.
Mpole aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na FC Lupopo ya DR Congo, anakumbukwa zaidi msimu wa 2021-2022, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akitupia mabao 17.