Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameipa majukumu makubwa Kamati Tendaji mpya ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu wake, Husna Abdallah, kuandaa rasimu ya ilani ya uchaguzi itakayoshawishi wananchi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Husna Abdallah, Katibu Mkuu wa sita wa chama hicho na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya CUF, atashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, pamoja na Ally Hamis, Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Zanzibar.
Viongozi hao walichaguliwa Januari 8, mwaka huu na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF katika mkutano mkuu baada ya majina yao kupendekezwa na Profesa Lipumba.
Akizungumza leo Jumapili, Januari 12, 2025 kuhusu majukumu ya kamati hiyo, Profesa Lipumba amesema Baraza Kuu la Uongozi limewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kukamilisha ilani hizo.
Amesisitiza kuwa ilani hiyo itazingatia maoni yanayoendana na haki sawa na ustawi wa kila mtu, kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Baraza Kuu la Uongozi limeagiza Katibu Mkuu na manaibu wake waendeleze kazi ya kukamilisha ilani ya Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, zikiakisi maoni ya haki sawa na furaha kwa wote,” amesema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba amesema ilani ya CUF kwa uchaguzi mkuu ujao itajikita katika maono na dira ya kuhakikisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi unakamilika, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwaondoa Watanzania katika hali ngumu ya maisha.
Amesisitiza kuwa changamoto ya ugumu wa maisha ni hoja iliyojadiliwa kwa kina na Baraza la Uongozi la CUF, ambalo limetoa mapendekezo ya suluhisho kutokana na kushindwa kwa chama kinachoongoza dola kuwainua wananchi licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali za taifa.
“Jukumu jingine muhimu ni kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unarudiwa chini ya usimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi, na wagombea wote wapate fursa ya kushiriki kwa usawa, kwani uchaguzi uliopita haukusimamiwa kwa haki na tumeazimia kwamba ufutwe,” amesema Profesa Lipumba.
Aidha, amesema ilani hiyo itaweka mkazo kwenye uwekezaji wa elimu bora ya msingi na sekondari kwa kila Mtanzania, huku wanafunzi wakifundishwa teknolojia na ujasiriamali tangu wakiwa shule ya msingi.
Amesema huduma za intaneti zinapaswa kupatikana kwa urahisi ili kuhakikisha kila kijana anayesoma ananufaika.
“Tunalenga kujenga uchumi wa soko shirikishi unapokua kwa wastani wa asilimia 10, kuongeza ajira nyingi na kuhakikisha kipato na furaha vinapatikana kwa usawa kwa wote,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Husna amesema amepokea maagizo hayo na ameanza kuandaa mpango wa utekelezaji kwa kushirikiana na wenzake.
“Wanachama na wajumbe waendelee kutuamini. Tutafanya kazi bora na tutashirikiana kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu,” amesema Husna.
Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, amesema Kamati Tendaji bado haijakamilika na watakutana na mwenyekiti wao wiki ijayo ili kukamilisha safu ya uongozi.
“Ni lazima baada ya kupatikana kwa Katibu Mkuu na manaibu wake, kamati iketi pamoja kukamilisha nafasi nyingine kama ya Mweka Hazina na Mkurugenzi wa Habari,” amesema Sakaya.
Kufukuzwa anachama Mtambile
Profesa Lipumba amethibitisha kuwa Baraza la Uongozi lilijadili na kuamua kumfukuza uanachama Mbunge wa Mtambile, Seif Salim Seif, baada ya kuonekana akitoa maneno ya hujuma na usaliti kupitia video.
“Katika video hiyo, Seif ameonekana akidai kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu na kwamba CCM kwake ni kama “jahazi analolazimika kulipanda ili asiangamie,” amesema Lipumba.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Seif kushindwa kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Uongozi ili ajitetee, licha ya kupewa wito rasmi.
“Baraza limeamua kwa kauli moja kumfukuza uanachama kwa mujibu wa Ibara ya 33, kifungu cha nne na tano cha Katiba ya CUF ya mwaka 1992, toleo la mwaka 2019,” amesema.
Mwananchi ilipomtafuta Seif kuzungumzia suala hilo, amesema hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia na kuahidi kutoa maoni yake baadaye.