Abalkassim freshi, Sebo bado kidogo

KLABU ya Pamba Jiji imekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa Fountain Gate, Abalkassim Suleiman kwa mkataba wa miaka miwili, huku uongozi ukiwa pia katika harakati za kuinasa saini ya beki wa kati wa Azam FC, Abdallah kheri Sebo.

Abalkassim amekamilisha usajili huo ikiwa ni mwezi mmoja tangu asimamishwe na Fountain Gate baada ya kushutumiwa kuihujumu timu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ulioshuhudiwa timu hiyo ikichapwa mabao 3-1 na Pamba Novemba 5, mwaka jana.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, nyota huyo alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 39, baada ya kumkanyaga nyota wa Pamba, Paulin Kasindi jambo lililomsababishia tuhuma hizo nzito.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha aliliambia Mwanaspoti, ni kweli wamempa mkataba wa miaka miwili nyota huyo kutokana na matakwa ya benchi la ufundi, huku akiweka wazi maboresho bado yanaendelea kikosini.

“Abalkassim ni mchezaji mzuri ambaye amependekezwa na kocha wetu, Fred Felix ‘Minziro’ hivyo nikiri wazi tumemsajili na hatuna shaka juu ya uwezo wake, bado tunaendelea kuboresha baadhi ya maeneo na tukikamilisha tutatangaza pia,” alisema.

Nyota wengine wapya waliojiunga na Pamba katika dirisha hili dogo la usajili ni, Deus Kaseke aliyewahi kuwika na Mbeya City na Yanga, Habib Kyombo, Hamad Majimengi na Mohamed Kamara waliotokea Singida BS kwa mkopo.

Wengine ni beki Mcameroon, Cherif Ibrahim kutoka Coton Sport, kiungo Mrundi Shassiri Nahimana aliyekuwa Bandari ya Kenya, winga Zabona Mayombya wa Tanzania Prisons na mshambuliaji Mkenya, Mathew Tegisi Momanyi aliyetokea Shabana FC.

Related Posts