Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia Junge Jilatu (28) na wenzake wawili, wakazi wa Kijiji cha Namsinde, Kata ya Mkulwe, Tarafa ya Kamsamba kwa tuhuma za mauaji ya watoto wake wawili.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga, leo Jumapili, Januari 12, 2025, imeeleza tukio hilo limetokea jana Jumamosi, Januari 11, 2025, saa 2:20 usiku nyumbani kwa mtuhumiwa. Hata hivyo, taarifa hiyo haijawataja watu wengine wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo
Kamanda Senga amedai kuwa mwanamke huyo aliwakaba watoto hao wakiwa wamelala na kuwakata kwa kitu chenye ncha kali shingoni, kisha mmoja ya watoto hao akamtupa kwenye mtaro wa maji kandokando ya barabara inayokwenda Namsinde.
Amewataja watoto waliouawa kuwa ni Lwambo Charles (3) na Kamba Charles mwenye miezi miwili.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo baada ya baba wa watoto hao kumtuhumu mtuhumiwa ambaye ni mke wake, kuwa amezaa na ndugu wa karibu kwenye familia yake. Uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani,” ameeleza Kamanda Senga.
Amewasihi wanandoa na wenza kutafuta suluhu ya migogoro yao kwa njia ya amani, ikiwemo kuwashirikisha wazazi na viongozi wa dini ili kuepuka madhara kama hayo. Amesema kitendo hicho ni ukatili na kinyume na haki za watoto na binadamu.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika wanafanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto,” amesisitiza Kamanda huyo.
Tukio hilo linatokea ikiwa umepita takribani mwezi mmoja ambapo Desemba 11, 2024, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro lilimkamata Teodora Mkunga (39), mkazi wa Lusange, Kata ya Mtombozi, Wilaya ya Morogoro, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake, Simon Gervas (8) kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake kwa panga.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Alex Mkama, alisema chanzo cha mauaji hayo ni mama kudaiwa kuwa na matatizo ya akili.
“Siku ya tukio, mama huyo alimvamia mtoto wake na kumshambulia kwa kutumia silaha yenye makali sehemu za kichwani na mgongoni, jambo lililosababisha mtoto huyo kupoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi,” alidai Kamanda Mkama.