Dar es Salaam. Moja ya mbinu za kujilinda dhidi ya wizi na utapeli unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii ni kutojibu maelekezo wala kutoa taarifa binafsi za mtumiaji kwa mtu ama chanzo asichokifahamu.
Kwa wale waliowahi kutapeliwa, ni dhahiri walikubali kwa namna moja ama nyingine kutoa taarifa zao binafsi, ikiwemo kuingiza nywila katika vyanzo visivyotambulika, wakati mwingine kwa kulaghaiwa hadi kupoteza pesa.
Wadau na wataalamu wa usalama mitandao pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamewataka wananchi kuwa makini na kujilinda dhidi ya uhalifu unaotekelezwa kwenye majukwaa ya kidijitali.
Mfano, moja ya umakini unaotakiwa, TCRA imesema ni kuhakiki vyanzo kabla ya kutekeleza maelekezo yanayotolewa mtandaoni, pamoja na kutojibu taarifa wanazotumiwa bila ridhaa zao kabla ya kuhakiki vyanzo hivyo.
Hatua hiyo inakuja kutokana na ongezeko la watumiaji wanaounganishwa mtandaoni. Hivyo, huduma salama za mtandaoni ni suala la msingi, hasa katika kutengeneza mtandao ulio salama kwa wote.
Huduma kama kupokea fedha kupitia simu za mkononi, kununua umeme, huduma za kielimu, matibabu, maji, na kuuza bidhaa za aina mbalimbali zinaweza kuvamiwa na watu wasio na nia njema, ikiwa ni pamoja na kuwaibia na kuwatapeli watumiaji.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Januari 12,2025 na Mwananchi, amesema mazingira salama mtandaoni yatawawezesha Watanzania kufikia malengo yao ya kiuchumi na ya uraia.
“Wananchi wanakumbushwa kuwa makini na kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni. Hii ni pamoja na kutotekeleza maelekezo wanayopewa na kutojibu taarifa wanazotumiwa bila ridhaa zao kabla ya kuhakiki vyanzo vyake,” amesema Dk Bakari.
Katika kutekeleza hilo, amesema mamlaka inaendelea kusisitiza kampeni kabambe ijulikanayo “Ni rahisi sana” inayolenga kuelimisha watu namna ya kubaini na kutambua matapeli na wezi mtandaoni.
Amesema kampeni hiyo itafanyika nchi nzima, ikilenga kuinua kiwango cha uelewa wa umma kuhusu fursa za mtandao wa intaneti na usalama wake.
Amesema kampeni hiyo ya awamu mbili, ilianza kutekelezwa Oktoba na Desemba mwaka jana na itaendelea kwa awamu ya pili, iliyoanza Januari na itadumu hadi Machi 2025 mtawalia.
Kampeni hiyo pia inahusisha namna ya kugundua maudhui mtandaoni yanayolenga kupotosha, na pia jinsi ya kugundua habari feki. Walengwa watafundishwa pia njia za kutoa taarifa za uhalifu mtandaoni.
Dk Bakari amesema mamlaka pia inawataka watu binafsi na taasisi kutumia zaidi kikoa cha Taifa (.tz) kwenye tovuti zao na anwani za barua pepe.
“Faida za kikoa cha Tanzania (.tz) ni pamoja na tovuti husika kupatikana kwa urahisi, salama zaidi dhidi ya udukuzi, na kutambulika utaifa wa huduma zinazotolewa hapa nchini Tanzania,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, Mwanamaudhui wa mtandao wa YouTube, Rashid Mansa, amesema elimu zaidi inahitajika kwa Watanzania licha ya hatua zaidi kuchukuliwa mbali na tahadhari hiyo.
“Watoe elimu kwa kutengeneza maudhui na watumie majukwaa yao ya TCRA kama Instagram ili watu waliopo hata vijijini elimu iwafikie,” ameshauri.
Kwa upande wake, Krantz Mwantepele, Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, amesema hiyo ni hatua muhimu katika kupambana na ongezeko la uhalifu wa mtandao ambao umekuwa ukisumbua watu wengi duniani hivi sasa.
“Kwa kuwa wananchi watakuwa waangalifu zaidi, itakuwa vigumu kwa wahalifu kufanikiwa katika mipango yao. Hii inasaidia kuimarisha usalama wa mtandao kwa ujumla,” amesema Mwantepele.