Adaiwa kuchoma nyumba kisa wivu wa mapenzi

Njombe. Mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina moja la Lino, anadaiwa kuchoma moto nyumba aliyopanga mpenzi wake, Ajentina Ngimbudzi (31) katika Mtaa wa Idundilanga, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Tukio hilo limetokea baada ya ugomvi uliosababishwa na madai ya wivu wa mapenzi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Januari 12, 2025, Ngimbudzi amedai ugomvi huo ulizuka jana saa 4 usiku baada ya Lino kufika kwenye biashara yake ya kuuza nyama na kumkuta huyo mwanaume amekaa jikoni.

“Mteja alikuwa amekaa jikoni, alipofika akauliza kwa nini yupo hapo. Nilimweleza kuwa ni mteja tu kama wateja wengine, lakini akaanza ugomvi. Mteja alikimbia, baada ya hapo Lino alikwenda nyumbani kwangu na kuwasha moto ulioteketeza baadhi ya nguo zangu na kusababisha nyumba kushika moto,” amedai Ngimbudzi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu kuhusiana na tukio hilo amesema linahusishwa na wivu wa mapenzi.

“Tunamtafuta mtuhumiwa aliyehusika na tukio hilo, ambaye kitendo chake kimesababisha hasara ya takriban Sh2 milioni, ,” amesema Kamanda Banga.

Tukio hili limelaaniwa na jamii, ikisisitizwa umuhimu wa kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia za amani badala ya kugeukia vitendo vya uharibifu.

Majirani, akiwemo Thadei Lugome, ameiambia Mwananchi kuwa alisikia kelele usiku akatoka na kwenda eneo la tukio ili kusaidia kuokoa mali. “Tulipiga simu kwa Jeshi la Zima Moto ambao walifika mapema na kusaidiana nasi kudhibiti moto. Tunalaani kitendo hiki cha kikatili kwa sababu kingeweza kusababisha vifo,” amesema Lugome.

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Njombe, Joel Mwakanyasa amesema; “Tathmini yetu imebaini chanzo cha moto ni matumizi ya mafuta. Tunatoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu ili kuepuka matukio ya aina hii.”

Mwakanyasa amesema nyumba hiyo ina vyumba vinane vya wapangaji, vitatu vimeteketea kabisa.

“Mpangaji wa pili alifanikiwa kuokoa baadhi ya vitu, ingawa vilikuwa tayari vimeharibiwa na moto,” amesema.

Related Posts