Dar es Salaam. Baada ya minyukano ya nguvu za hoja kwa takriban wiki mbili, uchaguzi wa viongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ngazi ya mabaraza, umeiva.
Mabaraza hayo ni vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha), ambayo yote uchaguzi wake unafanyika kesho Jumatatu, Januari 13, 2024.
Mkutano wa Bavicha utafanyikia ukumbi wa Ubungo Plaza huku wa Bazecha ukifanyika makao makuu ya Chadema.
Nafasi zinazowaniwa ni uenyekiti, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, katibu mkuu, manaibu wake wa Bara na Zanzibar, mweka hazina na waenezi wa mabaraza.
Uchaguzi huo utafuatiwa na wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), unaotarajiwa kufanyika Januari 16, mwaka huu.
Aidha, kutakuwa na wagombea wa mabaraza kuwania kuwa wajumbe wa mkutano mkuu.
Hata hivyo, wanazuoni wanasema uchaguzi katika mabaraza hayo matatu ni muhimu, kwa kuwa ndiyo unaowezesha kupatikana kwa viongozi watakaoamua uimara na kesho ya chama hicho.
Ukiachana na kiu ya ushindi aliyonayo kila mgombea, makundi ya wagombea uenyekiti wa chama kati ya lile linalomuunga mkono Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Freeman Mbowe na hasimu wake Tundu Lissu, ni jambo lingine linaloongeza joto la ushindani katika uchaguzi wa mabaraza hayo ambayo wagombea wake hasa wa nafasi ya uenyekiti wameshaonekana kuchukua upande kati ya Mbowe na Lissu.
Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti-Bara anachuana na Mbowe anayetaka kutetea kiti hicho alichokalia kwa miaka miongo miwili.
Nguvu na wingi wa wafuasi wa miamba hiyo miwili umesababisha kuzaliwa makundi mawili ndani ya Chadema na hivyo kuleta athari hata katika uchaguzi wa mabaraza.
Lissu mwenye falsafa ya mabadiliko ‘fikra mpya, mapambano mapya’ anaungwa mkono na mjumbe wa kamati kuu, John Heche anayewani umakamu mwenyekiti bara.
Mwenyekiti wa Kanda ya Viktoria, Ezekiel Wenje yeye anawania umakamu mwenyekiti bara akimuunga mkono Mbowe.
Uchaguzi wa mabaraza na taswira ya Chadema
Uchaguzi wa mabaraza unatajwa kwenda kutoa taswira ya timu hizo kati ya Mbowe na Lissu nani mwenye nguvu kuelekea uchaguzi mkuu wa chama utakaofanyika Januari 21, 2025, ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.
Kuelekea uchaguzi huo, tayari Kamati Kuu ya Chadema imeshaketi kwa siku tatu kuwafanyia usaili na kuwateuwa wagombea watakaoshindana katika nafasi hizo.
Duru za siasa zimekuwa zikiibua mijadala mbalimbali iwapo uongozi wa juu wa chama ukashinda upande mmoja na ule wa mabaraza ukashikiliwa na upande mwingine, hali itakuaje hasa kwa kuzingatia mnyukano wa wagombea wa kila upande.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza ameugusia uchaguzi huo akisema: “Hii timu Lissu/Heche dhidi ya timu Mbowe/Wenje ni kama mtego wa panya. Matokeo yakiwa Lissu/Wenje au Mbowe/Heche, demokrasia itaingia majaribuni. Bahati mbaya, ni rahisi kuingia mbinguni kuliko kusajili chama kipya Tanzania.”
Kiongozi huyo wa kiroho katika sehemu ya waraka wake kuelekea uchaguzi huo ameendelea kusema: “Ukweli mchungu: CCM inaihitaji CDM imara kuliko inavyolihitaji kundi moja ndani ya CDM.
CDM dhaifu ni sumu ya CCM. Na CDM inayahitaji mawazo ya mashabiki kuliko ya viongozi. Taifa imara linaihitaji CCM na CDM imara…’’
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kupitia taarifa yake ya leo Jumapili, Januari 12, 2025 walioteuliwa na kamati kuu kuwania uenyekiti wa Bazecha ni Hashim Juma Issa anayetetea nafasi hiyo, akichuana na wagombea wanne akiwemo Suzan Lyimo ambaye ni Makamu wake-bara.
Wengine kwenye nafasi hiyo, ni John Mwambigija, Hugo Kimaryo na Mwerchard Tiba.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Bara amejitokeza Shaban Madede pekee, huku Makamu Mwenyekiti Zanzibar ukiwaniwa na Mohamed Ayoub Haji na Hamoud Said Mohamed.
Walioteuliwa ukatibu mkuu wa Bazecha ni Dk Leonard Mao, Hellen Kayanza na Casmir Mabina ambaye amewahi kuwa Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani.
Upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara, wanaowania ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama, kwa upande wa Zanzibar ni Rajab Khamis Bakari ambaye ni mgombea pekee sawia na mweka hazina ambaye ni Florence Kasilima.
Katika uchaguzi wa Bavicha linaloongozwa kwa sasa na John Pambalu ambaye anamaliza muda wake kikatiba, wanaowania uenyekiti wa baraza hilo ni Deogratius Mahinyila, Hamis Masud na Shija Shibeshi.
Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, wanaowania ni Vitus Nkuna, Necto Kitiga, Juma Ng’itu, Nice Sumari na Mkolla Masoud.
Abdallah Rashid Haji ameteuliwa pekee nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar huku Benjamin Nteje, Idrisa Rubibi, Dua Lyamzito na Sheila Mchamba wakiutaka ukatibu mkuu.
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara wa Bavicha inawaniwa na Emanuela Kastuli na Revline Mbughi, huku Awena Nassor na Said Abdalla Hamis wakiwania kwa upande wa Zanzibar.
Ni wagombea wawili pekee ndiyo waliojitokeza kuutaka uratibu wa uhamasishaji ambao ni Felius Kinimi na Dedan Wangwe na nafasi ya Mweka Hazina inawindwa na Badi Ibrahim, Michael Materu na Rahima Abdallah.
Kamati kuu hiyo chini ya uenyekiti wa Mbowe imewateua watatu kuwania nafasi ya uenyekiti wa Baraza hilo kuchukua nafasi ya Halima Mdee ambaye alifukuzwa pamoja na wenzake kutokana na kukiuka miongozo ya chama.
Baada ya Mdee na wenzake 18 kufukuzwa Novemba 27, 2020 nafasi hiyo imekuwa ikikaimiwa na Makamu mwenyekiti, Sharifa Suleiman ambaye sasa ameteuliwa kuwania uenyekiti akichuana na wenzake wawili Celestine Simba aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Wananchi wa chama hicho.
Pia, kuna mjumbe wa kamati kuu Suzan Kiwanga aliyewahi kuwa mbunge wa Mlimba, Mkoa wa Morogoro. Makamu wenyeviti bara wameteuliwa saba ambao ni Agnes Chilulumo, Elizabeth Mwakimomo, Marietha Chenyenge, Moza Mushi, Naomi Ndigile, Rose Mkonyi na Salma Kasanzu.
Upande wa Zanzibar nafasi ya Makamu mwenyekiti wameteuliwa wawili ambao ni Bahati Chumu Haji na Zainabu Musa Bakari. Ukatibu mkuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na wanaowania akiwemo Catherine Ruge anayetetea nafasi hiyo. Wengine ni Esther Daffi na Pamela Maasay aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Glory Lataman, Neema Mhanuzi na Nuru Ndosi wameteuliwa pekee kuwania unaibu katibu mkuu-bara huku Asiata Said Aboubakar akiteuliwa nafasi hiyo upande wa Zanzibar. Benard Jonas na Joyce Mukya, aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum wakiteuliwa kugombea uweka hazina.
Akizungumza na gazeti hili, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Hadija Mwendah alisema uchaguzi huo ndiyo unaoamua kupatikana kwa viongozi wanaoamua uimara na kesho ya chama husika.
Hilo linatokana na kile alichofafanua, wazee ni muhimili wa kumbukumbu za utendaji wa taasisi na kupitia wao chama cha siasa kitakuwa na uwezo wa kurekebisha makosa yake kwa kuangalia matendo ya zamani.
“Wazee ni kama institutional memory (kumbukumbu ya taasisi) kutokana na umri wao wameyajua mengi na wanayaona yanayoendelea huwezi kurekebisha makosa, bila kujua ulipokosea zamani,” alisema.
Kwa upande wa vijana, alieleza ndilo kundi lililopo sasa na litakalokuwepo baadaye, hivyo ni kesho ya chama chochote cha siasa, wasipokuwepo leo, hawatajua lolote baadaye.
“Vijana ndiyo watenda kazi na ndiyo future na kama hawashiriki sasa inakosekana kujengwa misingi ya baadaye. Kwa hiyo uchaguzi wa vijana ni muhimu kwa sababu wao ndiyo kesho ya chama husika,” alieleza.
Kama ilivyo kwa wazee na vijana, Dk Hadija alisema wanawake pia ni walezi na ndilo kundi lenye mbinu za kutafuta kura na kushawishi wananchi.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, utatu wa makundi hayo ndio unaoleta maana ya chama cha siasa, jambo muhimu ni kuwashirikisha sio tu katika harakati, bali hata kwenye maamuzi.