Dar es Salaam. Mwanaharakati Maria Sarungi ambaye alidaiwa kutekwa leo nchini Kenya, amepatikana huku akiahidi kuzungumza zaidi kesho baada ya kutulia.
Taarifa ya kutekwa kwa Maria ilitolewa leo Jumapili Januari 12, 2025 na taasisi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ikisema: “Maria Sarungi Tsehai, mhariri huru wa vyombo vya habari nchini Tanzania na mtetezi wa haki za binadamu, ametekwa nyara na watu watatu wenye silaha katika eneo la Chaka, Kilimani jijini Nairobi.”
Katika video fupi iliyochapishwa katika ukurasa wa X (zamani Twitter) wa Faith Odhiambo ambaye pia ni rais wa 51 wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) imemuonesha Maria akiwa na Faith pamoja na watu wengine, huku Maria akiahidi kuzungumza kesho.
“Asanteni sana, nipo salama, Mungu ni mwema. Kesho nitachukua muda, nitaongea,niwashukuru Wakenya, Watanzania na watu wote wa kimataifa..Kwa sababu leo nimeokolewa,”amesema Maria