Yanga yaiua Al Hilal, matumaini yabakia Kwa Mkapa CAFCL

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga imefufua matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya usiku huu kushinda bao 1-0, dhidi ya Al Hilal, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Cheikha Ould Boidiya huko Nouakchott, Mauritania.

Katika mchezo huo wa hatua ya makundi mzunguko wa tano, Yanga ilipata bao la mapema tu dakika ya nane, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz KI aliyepiga shuti kali akipokea pasi ya Dickson Job na kumshinda kipa wa Al Hilal, Issa Fofana.

Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya dhidi ya Al Hilal baada ya kushuhudia mechi ya kwanza tu ya ufunguzi wa kundi ‘A’, kuchapwa mabao 2-0, jijini Dar es Salaam Novemba 26, mwaka jana hivyo kulipa kisasi kwa Wasudani hao.

Timu zote zilicheza kwa kushambuliana huku zikikosa utulivu wa kumalizia nafasi zilizotengenezwa ingawa katika dakika 45 za kwanza, Yanga ilionekana zaidi kuutawala mchezo ambapo iliutawala kwa asilimia 53, dhidi ya 47 za wapinzani wao.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza Yanga ilionyesha kuuhitaji mchezo huo ambapo ilitengeneza nafasi tatu zilizolenga lango na kupata bao moja huku kwa upande wa wapinzani wao wakishindwa kufurukuta licha ya kiwango bora cha Jean Claude Girumugisha.

Kipindi cha pili timu zote pia ziliendelea kushambuliana ambapo licha ya Yanga kuongoza na kutaka mabao zaidi ila ilicheza kwa nidhamu ya kujilinda, huku kwa upande wa Al Hilal ikishambulia ili kusawazisha bila ya mafanikio yoyote.

Ushindi huo wa Yanga ni wa pili mfululizo katika kundi hilo baada ya Januari 4, kuichapa TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1, jijini Dar es Salaam, hivyo kuweka matumaini hai ya kutinga hatua ya robo fainali kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Ushindi huo sio kwamba tu umeweka matumaini hai ya Yanga kutinga hatua ya robo fainali, bali ni wa kwanza kwake dhidi ya Al Hilal kwenye michuano ya CAF, hivyo kikosi hicho kinachonolewa na Mjerumani Sead Ramovic kuweka pia rekodi ya kibabe.

Yanga inafikisha jumla ya pointi saba katika kundi ‘A’, ikihitaji ushindi wa aina yoyote katika mchezo ujao wa Januari 18 dhidi ya MC Alger ya Algeria yenye nane, huku Al Hilal ambao ni vinara wakiwa na pointi 10 wakiwa tayari wamefuzu.

Kikosi kilichoanza Al Hilal: Issa Fofana, Altayed Abdelrazig, Jean Claude Girumugisha, Aime Tendeng/ Abdelrazig Yagoub Omer Taha, Mohamed Abdelrahman/ Yaser Muzmel Muhamed, Adama Coulibaly/ Serge Pokou, Khadim Diaw, El Hadji Madicke Kane/ Salaheldin Adil Ahmed, Steven Ebuela Ehebelo, Guessouma Fofana, Ousmane Diouf.

Kikosi kilichoanza Yanga: Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua/ Clatous Chama, Mudathir Yahya/ Duke Abuya, Stephane Aziz KI/ Kennedy Musonda, Clement Mzize, Prince Dube.

Related Posts