Hatma kesi ya Dk Slaa kujulikana leo

Dar es Salaam. Vigogo hawa leo Jumatatu Januari 13, 2025 wanatarajia kupishana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Miongoni mwa vigogo hao ni wanasiasa mkongwe, Wilbroad Slaa (76), ambaye anakabiliwa shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X zamani Twitter.

Dk Slaa alifikishwa mahakamani hapo, Ijumaa ya Januari 10, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025 na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato akishirikiana na Tumaini Mafuru na Abdul Bundala.

Dk Slaa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Mshtakiwa huyo alisomewa shitaka lake mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Wakili Kato alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, kesi hiyo leo Jumatatu inakuja kwa kujadili dhamana baada ya Serikali kuzuia dhamana yake kwa kuwasilisha maombi na kiapo cha kuzuia dhamana.

Kesi nyingine itakayotajwa leo ni ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Kwa mara ya kwanza Gasaya, alifikishwa Mahakamani hapo Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Hata hivyo, tangu siku hiyo hadi leo, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na mshtakiwa yupo rumande hana dhamana kutoka na shitaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, Gasaya anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.13 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.

Pia anadaiwa kutakatisha fedha kiasi hicho cha fedha na kwamba kesi hiyo inasikilizwa mbele ye Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.

Wakati huohuo, kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wamiliki watatu wa jengo lililoporomoka mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, itatajwa mahakamani hapo.

Wamiliki hao, ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala.

Mdete na wenzake wanakabiliwa na mashitaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 24, 2024 na kusomewa kesi hiyo.

Katika hatua nyingine, kesi ya kusafirisha kilo 332 za heroini na Methamphetamine  inayomkabili, mvuvi wa samaki Ally Ally(28), maarufu Kabaisa na wenzake wanane, itatajwa mahakamani hapo.

Mbali na Ally, washtakiwa wengine ni Bilal Hafidhi (31)ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis (47) mvuvi wa samaki na  Idrisa Mbona (33) ambaye ni  muuza magari.

Wengine ni Rashid Rashid (24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji; Shabega Shabega(24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.

Pia, yupo Dunia Mkambilah(52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke;  mfanyabiashara Mussa Husein (35)mkazi wa Mwambani na Hamis Omary(25).

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Aprili 22, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Washtakiwa wapo rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria na pia upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Kesi ya tano itakayotajwa mahakamani hapo ni ya kughushi kitambulisho cha Taifa (Nida) na kitambulisho cha mpigakura, inayomkabili raia wa Burundi, Kabura Kossan(65).

Kabura anakabiliwa na jumla ya mashitaka sita yakiwemo kutakatisha fedha kiasi cha Sh8 milioni zilizotokana na kununua eneo lenye ukubwa wa ekari 100 lililopo kijiji cha Kibesa, Wilaya ya Mkuranga.

Mshtakiwa anakabiliwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 24289/ 2024 na ipo katika hatua ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, na mshtakiwa yupo rumande kutokana shitaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana.

Related Posts