Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewapongeza wagombea wote wanaoshiriki uchaguzi wa ndani wa chama hicho, huku akiwakumbusha mambo matatu ikiwemo kuilinda taasisi yao.
Mbowe amechapisha ujumbe huo katika kurasa zake za mitandao ya kijamii leo Jumatatu, Januari 13, 2025 kuelekea uchaguzi wa mabaraza ya vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha), ambayo uchaguzi wake unafanyika leo.
“Leo ni siku muhimu sana kwa Chadema tunapofanya uchaguzi wetu wa ndani kwa ajili ya mabaraza ya wazee na vijana. Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wagombea wote wanaoshiriki. Kila mmoja wenu ni wa thamani kwetu katika kupigania maono ya chama chetu,” ameandika Mbowe na kuongeza;
“Katika safari yetu hii, hebu tukumbuke kwamba uchaguzi huu ni zaidi ya nafasi; ni kuhusu kuunda mustakabali mzuri kwa Chadema na kwa Taifa letu. Sote tuna jukumu la kuilinda taasisi yetu na kuhakikisha tunamaliza hatua hii tukiwa imara zaidi.”
“Ninawahimiza wanachama na wafuasi wote kufuatilia mchakato huu wa kidemokrasia ndani ya chama chao. Pamoja, tukiwa na umoja, tutaweza kufanikisha mambo makubwa. Tunaposhirikiana, tunaweza kujenga Chadema yenye nguvu zaidi kwa sababu yeyote atakayechaguliwa, Chadema imeshinda!”
Endelea kufuatilia Mwananchi.