Akandwanaho anatua Tabora United | Mwanaspoti

UNAMKUMBUKA  Joseph Akandwanaho aliyekodishwa na Mlandege katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na kuitibulia Simba kwa kufunga bao pekee lililowakosesha Wekundu taji la tano la michuano hiyo? Sasa jamaa anajiandaa kutua Tabora United iliyomkosa katika dirisha kubwa la usajili.

Kiungo mshambuliaji huyo aliyeichezea Mlandege katika fainali hizo za mwaka jana na kuiwezesha timu hiyo ya Zanzibar kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo, ni mali la Mbarara City ya Uganda na Tabora ilivutiwa na kiwango chake na kutaka kumsajili dirisha lililopita, lakini mambo yakakwama.

Hata hivyo, safari hii Tabora imemrudia tena na inadaiwa kwa sasa ipo hatua ya mwisho kumsainisha mkataba ili aitumikie timu hiyo katika ngwe ya pili ya Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Tabora kimeliambia Mwanaspoti kuwa taratibu zote za kumnasa nyota huyo Mbarara City ya Uganda zimekamilika kilichobaki ni staa huyo kusaini tu mkataba.

“Ni kweli baada ya kamkosa katika dirisha kubwa sasa mazungumzo ya pande zote mbili yanakwenda vizuri na muda wowote kuanzia sasa kabla ya dirisha la usajili kufungwa atakuwa amekamilisha kila kitu,” kilisema chanzo hicho kutoka Tabora United na kuongeza;

“Bado tunaendelea kuboresha kikosi chetu licha ya kufanya vizuri mzunguko wa kwanza, tunahitaji kuongeza nguvu kwenye nafasi mbalimbali ili mzunguko wa pili utakaporejea Machi tuendelee tulipoishia.”

Inaelezwa Akandwanaho ambaye ndiye nahodha amebakiza mkataba wa miezi sita katika klabu ya Mbarara kwa sasa ikishika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uganda inayoshirikisha timu 16, ikivuna pointi 14 mechi 15.

Related Posts