Zubery Katwila avuta mashine tatu Bigman

KOCHA wa Bigman FC, Zubery Katwila ameanza kukisuka kikosi hicho baada ya kuzinasa saini za aliyekuwa beki wa kulia wa African Sports, Halfan Mbaruku, kiungo, Abubakar Hamis na mshambuliaji, Rafael Siame waliojiunga wakiwa wachezaji huru. 

Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila alisema bado hajapata taarifa rasmi za nyota wapya waliosajiliwa na viongozi wa timu hiyo, ingawa mojawapo ya mapendekezo yake aliyoyapendekeza ni kuongezewa nguvu maeneo ya kiungo mkabaji na mshambuliaji.

“Siwezi kusema moja kwa moja kama wachezaji uliowataja tumefanikisha usajili wao kwa sababu sijapata taarifa zao, kama ni kweli viongozi wenyewe wataweka wazi, ingawa ni kweli ripoti yangu nilishaiwasilisha na inafanyiwa kazi,” alisema.

Kocha huyo mzoefu aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar, amejiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’, aliyejiunga na Pamba kuchukua mikoba ya Goran Kopunovic.

Timu hiyo zamani iliyofahamika kama Mwadui FC ambayo imehamia Lindi, katika michezo 15 iliyocheza imeshinda sita, sare minne na kupoteza mitano, ikifunga mabao 11 na kuruhusu pia 11, ikishika nafasi ya nane kwenye msimamo na pointi 22.

Related Posts