KIUNGO mshambuliaji raia wa Tanzania, Bernard Kamungo amepata shavu la kuongeza mkataba wa miaka mitatu hadi 2028 katika klabu yake ya FC Dallas ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Nyota huyo mzaliwa wa Congo aliyekulia katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, Tanzania maisha yake ya soka amekulia Marekani akitumikia klabu ya North Texas (2021/22) ya Ligi Daraja la Tatu ambako kwenye mechi 52 alifunga mabao 22.
Msimu uliofuata akajiunga na Dallas aliposaini mkataba wa miaka miwili na msimu wa kwanza amefunga mabao sita kwenye mechi 36 alizocheza.
Taarifa zilizochapishwa kwenye ukurasa wa Dallas zimeeleza: “Tumemuongezea mkataba mpya wa miaka mitatu kiungo wetu Bernard Kamungo, ukiwa na chaguo la klabu kwa mwaka 2027 na 2028,” ilisomeka taarifa hiyo.
Baada ya kuonyesha kiwango bora ndani ya kipindi hicho na kuwa miongoni mwa wachezaji wanaozungumzwa nchini humo, Dallas ikamuongezea mkataba wa miaka mitatu wenye kipengele cha kuongeza mwingine.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 22, amekuwa mchezaji muhimu wa Dallas kwa kasi ya ajabu ndani ya mwaka mmoja na nusu uliopita.
Kati ya mabao yake sita aliyofunga msimu uliopita kwenye Ligi ya MLS, mawili yalikuwa ya ushindi, mawili ya kusawazisha, na mawili yalikuja kwenye ushindi wa 4-1 wa Dallas dhidi ya LA Galaxy, mechi muhimu iliyowahakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano.
Alifunga bao dhidi ya Inter Miami ya Lionel Messi, siku ambayo mshindi huyo mara saba wa Balon d’Or alifunga mabao mawili katika mechi yao ya hatua ya 16-Bora ya Kombe la Ligi iliyomalizika kwa mabao 4-4, kablaya kina Messi kushinda kwa penalti 3-2.
Akimzungumzia, kocha wa Dallas, Mmarekani Eric Quill alisema Kamungo ni mpambanaji akiwa uwanjani.
”Anadhihirisha tabia na akili thabiti kama mchezaji, hajali ni mpinzani wala hali gani ya mchezo anaingia uwanjani na kushindana, na hiyo ndiyo njia bora zaidi kwake kufanya hivyo,” alisema Quill.