Kikosi cha zimamoto na uokoaji nchini Marekani Jumapili ya Januari 12, 2025 kililazimika kuongeza kasi ya kukabiliana na moto wa nyika ulioangamiza maelfu ya nyumba na kusababisha vifo vya watu 24 Los Angeles baada ya watabiri wa hali ya hewa kuonya kuhusu upepo mkali unaotarajiwa kuanza tena wiki hii.
Watu wasiopungua 16 bado hawajulikani walipo ambapo mamlaka zimesema idadi hiyo huenda ikaongezeka.
Mamlaka ya hali ya hewa nchini humo imetoa tahadhari ya juu kuwa maafa ya moto yanaweza kuongezeka kwa kasi hadi Jumatano kutokana na upepo unaotarajiwa kuwa na kasi ya hadi kilometa 80 kwa saa na upepo mkali milimani unaotarajiwa kufikia kilometa 113 kwa saa (113 kph).
Kwa mujibu wa mtabiri wa hali ya hewa, Rich Thompson Jumanne ya Januari 13, 2025 inatarajiwa kuwa siku hatari zaidi.
“Kutakuwa na upepo mkali wa Santa Ana, hali ya hewa kavu, na nyasi zenye ukame mkubwa, hivyo tunatarajia hali hatari ya moto,” Thompson alisema katika mkutano na wanajamii Jumamosi usiku.
Mkuu wa Zimamoto wa Kaunti ya Los Angeles, Anthony Marrone, alisema kwamba magari 70 ya ziada ya maji yalifika kusaidia kuzima moto unaosambazwa na upepo.