Los Angeles. Moto wa nyika umeendelea kuwa mwiba kwa wakazi na maofisa wa Kikosi cha Zimamoto jijini Los Angeles, Marekani, baada ya vifo kuongezeka na kufikia watu 24.
Zimamoto pia imetahadharisha kuwa huenda idadi ya waliofariki kutokana na moto huo ulioibuka Januari 9, 2025, ikaongezeka kwa kile kinachotajwa kuwa bado ufuatiliaji unaendelea ili kujua madhara katika maeneo ambayo moto bado unaendelea kuteketeza.
Tovuti ya BBC imeripoti kuwa wakati huu ambapo jitihada za kuudhibiti hazijazaa matunda, kunahofiwa kuibuka upepo mkali hususan eneo la Santa Ana kuanzia jana Jumapili hadi Jumatano wiki hii, utakaokuwa ukivuma kwa wastani wa kasi ya kilomita 96 kwa saa.
Pamoja na moto huo kuendelea kuteketeza maeneo ya vilima vya Hollywood, jitihada za zimamoto zinaonekana kuzaa matunda baada ya kuupunguza nguvu hususan katika maeneo ya Palisades na Eaton.
Tayari maofisa wa zimamoto kutoka Marekani wameongezewa nguvu na mamia ya wataalamu wa kuzima moto kutoka Canada na Mexico, ambao wameendelea kuwasili nchini humo.
Ofisi ya Usimamizi wa Afya jijini Los Angeles imetoa taarifa kuwa waliofariki hadi leo Jumatatu, Januari 13, 2025, ni watu 24 huku 16 wakiwa hawajulikani walipo.
Kati ya waliofariki, watu 16 waliteketea katika moto uliounguza eneo la Eaton, huku wanane wakifariki katika moto uliounguza eneo la Palisades jijini humo.
Hadi sasa kuna moto katika maeneo matatu ya Jiji la Los Angeles ambao bado ni tishio kwa raia wa Marekani.
Moto mkubwa kati yao uko eneo la Palisades, ambapo takwimu za zimamoto zinaonyesha hadi sasa umeteketeza ekari zaidi ya 23,000, huku asilimia 11 ya moto huo ikiwa imedhibitiwa.
Moto uliozuka eneo la Eaton jijini humo unatajwa kuwa wa pili kwa ukubwa na hatari, ambapo hadi leo umeteketeza ekari 14,000, japo asilimia 27 imeshadhibitiwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa moto ulioibukia eneo la Hurst kwa takribani ekari 799 umekaribia kudhibitiwa na kuzimwa kabisa kwa jitihada za vikosi vya zimamoto kutoka mataifa hayo.
Jana Jumapili, Taasisi binafsi ya utabiri wa hali ya hewa, Accuweather, ilidai kuwa hasara iliyosababishwa na moto huo katika mali na makazi huenda imefikia kati ya Dola bilioni 250 za Marekani (Sh631.25 trilioni) hadi Dola bilioni 275 (Sh694.37 trilioni).
Mamlaka hiyo pia imeonya hatari ya moto huo kusambaa maeneo mengi ya Jimbo la Los Angeles endapo upepo unaotarajiwa utapuliza kwa kasi na usipodhibitiwa kwa wakati, hivyo kuwataka wananchi kuongeza umakini wakati huu.
“Kwa bahati mbaya, tunalazimika kutoa taarifa mbaya kuwa huenda tukapitia wakati ambao kuna moto wenye madhara zaidi katika kipindi cha Jumapili hadi Jumatano kutokana na upepo unaotarajiwa kupuliza katika siku hizo,” amesema Mkuu wa Zimamoto eneo la Pasadena, Chad Augustin.
“Pamoja na kuwa tunaendelea kuudhibiti, bado hakuna dalili za kuushinda hadi sasa,” ameongeza.
Kristin Crowley, Mkuu wa Zimamoto jijini Los Angeles, amewataka wananchi walioondolewa katika makazi yao kutorejea katika maeneo hayo hadi pale itakapotangazwa vinginevyo.
Mkazi wa Bonde la Topanga jijini humo, Alice Husum (67), ameieleza BBC kuwa kuna moto umeonekana kuibuka eneo hilo usiku wa kuamkia leo, jambo ambalo limeibua taharuki kwake na kwa majirani zake kuhusu hatma ya makazi yao.
Jana, zimamoto walifanikiwa kuudhibiti moto huo usifike ulipo Msitu wa Taifa wa Los Angeles, eneo ambalo ndiko kuna Kituo cha Taifa cha Usafirishaji wa Anga.
Takwimu zinaonyesha kuwa watu 29 wanashikiliwa kwa madai ya kufanya uharibifu na udokozi wa mali za waathiriwa wa janga hilo, hususan katika maeneo ambayo wakazi wametakiwa kuondoka.
Mkuu wa Jeshi la Nchi hiyo jijini Los Angeles, Robert Luna, amesema ulinzi umeimarishwa katika eneo lenye makazi ya waathiriwa wa moto huo, na tayari askari wa jeshi la nchi hiyo zaidi ya 400 wamemwagwa eneo lote kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Gavana wa California, Gavin Newsom, ametangaza kuwa askari wa jeshi la nchi hiyo 1,000 wataongezwa ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Hadi sasa, maofisa wa zimamoto zaidi ya 14,000 wamefika eneo la Kusini mwa California, wakisaidiwa na ndege 84 na mashine za kuzima moto 1,354.
Idadi ya walioamriwa kuyaacha makazi yao inakadiriwa kuwa ni watu 105,000, huku zaidi ya 87,000 wakiwa hatarini kuhamishwa kwa sababu ya tishio la moto huo.
Msimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Uratibu wa Majanga (FEMA) nchini humo, Deanne Criswell, amesema bado kuna tishio la moto huo katika usalama wa binadamu.
“Natambua kwamba watu wengi wanahitaji kurejea kwenye makazi yao na kuangalia hali ya makazi yao, lakini bado kuna tishio la upepo mkali unaoweza kuhatarisha usalama wao,” amesema Criswell.
Mkuu wa Idara ya Polisi Los Angeles (LAPD), Jim McDonnell, amesema jeshi hilo limeweka zuio la muda kwa sasa kwa wakazi wa eneo hilo kurejea, ili kuwakinga dhidi ya hatari wanayoweza kuipata.
Wakati huohuo, mvutano kati ya Gavana wa California na Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, unaendelea baada ya kiongozi huyo anayetarajiwa kuapishwa Januari 20 mwaka huu kudai kuwa uzembe umechangia kuongezeka kwa janga hilo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.