Mume adaiwa kumuua mkewe kwa kumchinja shingoni

Babati. Shabani Rajabu (60), mkazi wa Kijiji cha Maweni, Kata ya Magara, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, anadaiwa kumuua mkewe, Zulfa Rajabu (40), kwa kumchinja shingoni na kumkata mkono.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo na wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maweni A, Zakaria Serea, amesema tukio hilo lilitokea Januari 11, 2025, katika kitongoji hicho.

Amesema mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa na majeraha ya kutisha, na shingo ikiwa imekatwa pamoja na majeraha mengine mwilini.

Inadaiwa Rajabu alimchinja mkewe, Zulfa, kwa kutumia kisu baada ya kutokea ugomvi kati yao.

Mwenyekiti huyo wa kitongoji amewataka wakazi wa eneo hilo kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kutafuta suluhisho la amani katika migogoro ya kifamilia.

Baadhi ya majirani wa familia hiyo wamelaani tukio hilo, ambalo limeacha simanzi kubwa hasa kwa watoto watatu wa familia hiyo, ambao bado ni wadogo.

Ndugu wa marehemu, Abdilahi Ismail, amedai chanzo cha mauaji hayo ni ulevi na wivu wa kimapenzi.

Ismail amesema polisi walifika eneo la tukio, walichukua mwili wa marehemu, na kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Magara.

Tukio hilo limeongeza idadi ya matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Manyara.

Related Posts