HABARI zinabainisha kwamba Dodoma Jiji imekamilisha usajili wa beki Mukrim Issa aliyekuwa akiitumikia Coastal Union tangu mwanzo wa msimu huu.
Beki huyo alikuwa akiichezea Coastal Union kwa mkopo akitokea Singida Black Stars na sasa amepelekwa tena Dodoma Jiji kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa, dili hilo tayari limekamilika na mara baada ya ligi kurejea Machi Mosi mwaka huu beki huyo atakuwa sehemu ya kikosi cha Dodoma Jiji.
Mukrim anakwenda kuwania namba na aliyewahi kuwa beki wa Simba, Joash Onyango ambaye alijiunga na timu hiyo dirisha kubwa la usajili. Wengine wanaocheza eneo hilo la beki wa kati ni Augustino Samson na Lulihoshi Heritier.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza amesema beki huyo kupelekwa kwa mkopo Dodoma Jiji na kuweka wazi kuwa muda wowote taarifa kuhusiana na mchezaji huyo zitatolewa.
“Mukrim ni kweli ameombwa na Dodoma Jiji na ataungana na timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita ili kwenda kukuza uwezo wake na tunaamini atapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza,” alisema.