Mawakili waibua jambo kesi inayomkabili Dk Slaa

Dar es Salaam. Wakati Jamhuri ikiwasilisha pingamizi la dhamana dhidi ya mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbrod Slaa, anayekabiliwa na kesi ya jinai, mawakili wake pia wameibua pingamizi dhidi ya kesi hiyo wakihoji uhalali wake.

Jopo la mawakili wa Dk Slaa linaloundwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na mawakili wengine maarufu wakiwamo Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Sisty Aloys na Sanga Melikiori, wameibua pingamizi hilo leo Jumatatu, Januari 13, 2025.

Kesi hiyo ilipangwa leo kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi la dhamana lililowasilishwa na upande wa mashtaka, lakini kabla ya kusikilizwa kwa pingamizi hilo, mawakili hao wakaibua pingamizi dhidi ya shtaka linalomkabili wakihoji uhalali wa kesi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, mshtakiwa Dk Slaa ambaye yuko mahabusu katika Gereza la Keko hakuwepo mahakamani na hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu kutokufikishwa mahakamani.

Awali, Dk Slaa alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, Ijumaa, Januari 10, 2025 na kusomewa shtaka moja.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 993 ya mwaka 2025, Dk Slaa  anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa X zamani Twitter,  kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anadaiwa siku hiyo ya tukio, kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai ameandika ujumbe uliosomeka:

“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya … na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa  ni dhahiri atatoa pesa … hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”

Pia, anadaiwa kuandika katika akaunti maneno yalisomeka kama: “Samia toka muda mrefu hahangaiki tena na maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe,” wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.

Hata hivyo, Dk Slaa alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa,  upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mwasipu alidai kuwa, shtaka linalomkabili mteja wao linadhaminika, hivyo akaiomba Mahakama itoe masharti nafuu ya dhamana.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Clemence Kato alidai kuwa, Serikali imewasilisha maombi ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo, yaliyoambatanishwa na kiapo ilichoandaliwa na mpelelezi wa kesi hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP ) George Wilbroad Bagyemu.

“Kiapo hiki kimewasilisha mahakamani hapa chini ya kifungu 148 (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.  Tayari tumekiwasilisha katika mfumo wa mtandao katika Mahakama yako,” alidai Kato.

Wakili Mwasipu alipinga maombi hayo akidai kuwa, hawajapatiwa nakala ya kiapo hicho na hakuna uhakika kama kimesajiliwa kwenye mfumo wa Mahakama.

Baada ya mvutano huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki anayesikiliza kesi hiyo aliahirisha kesi hiyo mpaka leo kwa ajili ya kujadili maombi hayo ya Serikali kupinga dhamana.

Hata hivyo, kesi hiyo ilipotajwa leo, Dk Slaa hakuwepo mahakamani na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa kwanza ameieleza Mahakama kuwa, mshtakiwa hajafika na hawana taarifa kwani nini hajafika.

Akizungumzia taarifa hiyo, Madeleka ameeleza kushangazwa na upande wa mashtaka kutokujua kwa nini mshtakiwa hajafikishwa mahakamani wakati wao ndio wenye wajibu wa kumfikisha mahakamani, kwa mshtakiwa ambaye yuko mahabusu.

Wakili Madeleka ameiomba Mahakama ijiridhishe na hali yake kwa kuwa, hakuna anayejua kama huko aliko yuko salama ama la, huku akiomba upande wa mashtaka uwajibike kwa hilo.

Hata hivyo, Wakili Mwabukusi ameiomba Mahakama kuendelea hata kama mshtakiwa hayupo.

Wakili Issa ameikumbusha Mahakama kuwa, wamewasilisha maombi ya kupinga dhamana kwa hati ya faragha (hati ya maombi) na kiapo na wanategemea kupata kiapo kinzani kutoka kwa mujibu maombi kisha wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji.

Hoja hiyo ilipingwa na wakili Madeleka akisema kuwa, wapo tayari kuwapa kiapo kinzani waendelee kusikilizwa na kama Mahakama itaona haiwezi kusikiliza maombi hayo, iendelee na usikilizwaji wa masharti ya dhaman.

Hata hivyo, Hakimu Nyaki ameelekeza kuwa, maombi ya kupinga dhamana yasikilizwe na kuamuriwa ndipo aendelee na kesi ya msingi.

Kutokana na uamuzi huo, wakili Madeleka akaibua pingamizi dhidi ya kesi hiyo akihoji uhalali wake.

Madeleka amesema kuwa, chini ya kifungu cha 131A cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022, hakuna kesi itakayofunguliwa kabla ya upelelezi kukamilika isipokuwa kama ni makosa makubwa.

“Kwenye kumbukumbu zangu, nilisikia walisema upelelezi haujakamilika, kwa hiyo kesi hiyo na yote yanayoendelea ni batili na haipaswi kuwepo mahakamani pamoja na hayo maombi,” amesema Madeleka.

Ameiomba Mahakama ikubali kupokea pingamizi lao kwa njia ya mdomo chini ya kifungu cha 392 (1) CPA kinachoruhusu kuleta pingamizi kwa mdomo na wapangiwe kuisikiliza keshokutwa Jumatano.

Wakili Kato amesema hawana pingamizi na usikilizwaji wa pingamizi la upande wa utetezi, lakini akaomba wapangiwe kusikiliza pingamizi la utetezi Ijumaa, Januari 17, 2025 akidai Jumatano mawakili wengi watakuwa kwenye kesi nyingine za uhujumu uchumi.

Hoja hiyo imepingwa na wakili Madeleka akidai hiyo sababu haina mashiko maana ofisi ya mashtaka ni taasisi na ina mawakili wengi.

“Vinginevyo watutajie hicho kifungu,”, amesisitiza wakili Madeleka.

Hata hivyo, baada ya mvutano wa hoja hiyo, Hakimu Nyaki amekubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo mpaka Ijumaa Januari 17, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi ya Serikali kupinga dhamana na pingamizi la utetezi dhidi ya uhalali wa kesi hiyo.

Related Posts