Arusha. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha, kimeanza msako wa kuwakamata madereva wote waliokaidi kupeleka magari yanayobeba wanafunzi.
Imeelezwa kuwa madereva hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Ukaguzi huo ulianza Desemba mwaka jana wakati shule zimefungwa lengo ni kutaka kuondokana na ajali zinazosababishwa na ubovu wa vyombo hivyo vya moto.
Akizungumza leo Jumatatu Januari 13, 2025, Mkuu wa Kikosi hicho mkoani Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Zauda Mohamed, amesema baada ya kuhitimisha kwa ukaguzi huo, leo wameanza kuyakamata magari yote ambayo hayajakaguliwa.
Amesema kikosi hicho kilishatangaza Januri 13, (leo) kinaanza rasmi operesheni ya kuwasaka wote ambao hawakupeleka magari hayo kukaguliwa kama ilivyoagizwa.
Kamanda Mohamed amesema takwimu za mkoa huo zinaonesha kuna magari 563ya shule yanayobeba wanafunzi lakini baada ya kazi ya ukaguzi kukamilika, imebainika kuna magari 178 hayajakaguliwa.
“Baada ya kukamilisha ratiba yetu ya ukaguzi wa magari ya shule, leo tumeanza msako mkali wa kuwakamata wale wote waliokaidi kuleta vyombo vyao kukaguliwa katika vituo vyetu vya polisi,” amesema kamanda huyo.
Hivyo, ametoa wito kwa wamiliki wote ambao hawajapeleka mabasi hayo kukaguliwa, wasianze kazi ya kuwasafirisha wanafunzi mpaka yatakapokaguliwa.
Amesema lengo la ukaguzi huo ni kutaka kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Lakini pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwaelekeza wanafunzi hususan wa shule za awali na msingi, matumizi sahihi ya barabara pindi waendapo shule na kurejea nyumbani.
“Wazazi tuhakikishe tunawalinda watoto wetu hasa hawa wanaoanza shule, msiwaache peke yao barabarani, bado hawajayajua mazingira salama ya kutembea barabarani. Tunapokutana na kundi hili tuwasaidie pia wapite au wavuke salama barabara,”amesema Mohamed.
Pia, ametoa wito kwa madereva kuhakikisha katika kipindi hiki ambacho shule zimefunguliwa, wawe waangalifu wanapopita barabarani wajue kuna kundi jipya barabarani ambalo linatakiwa uangalizi mkubwa.
Naye Joachim Paskali mmoja wa wazazi kutoka Kata ya Elerai jijini hapa, amesema ukaguzi huo ni muhimu ufanyike mara kwa mara kwa sababu utasaidia kupunguza ajali zinazoepukika za magari yanayobeba wanafunzi.
“Tunalipongeza jeshi la polisi kwa ukaguzi huu maalum kwa magari yanayobeba wanafunzi, hii inatuhakikishia sisi kama wazazi kuwa watoto wetu wanapanda vyombo vya moto vilivyo salama ila tunaomba ukaguzi huu uwe endelevu,” amesema Paskali.
Akizungumzia hilo, Joan Lukumay mkazi wa Arusha mjini, amesema hatua hiyo ni nzuri kwa sababu magari mengi ya shule ni mabovu.
“Tunalipa ada ya usafiri lakini magari mengi ya shule ni mabovu, hayafanywi matengenezo hali inayochangia uwepo wa ajli zinazogharimu maisha ya watoto wetu,” amesema.
Hivyo ameliomba Jeshi la Polisi linapofanya ukaguzi huo, liangalie pia suala laujazaji wa wanafunzi kwenye magari hayo.
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Tanzania (Tamongsco),Yusto Ntungi amesema ubora wa usafiri kwa wanafunzi ni kipaumbele chao, lakini changamoto kubwa ni ubovu wa barabara za mitaani.
Amesema wamekuwa wakiwasilisha kero hiyo kwenye vikao vyao na mamlaka za Serikali, lakini utatuzi wake umekuwa kitendawili.