Vitambulisho 31,000 vya Nida vilivyofutika kutengenezwa upya

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema alishatoa maagizo kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kutengeneza upya vitambulisho takribani 31,000 vilivyofutika taarifa zake.

Waziri huyo amesema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na ubora hafifu wa vitambulisho hivyo na kuagiza vitengenezwe upya.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Januari 13, 2025 kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Wizara ya Mambo ya Ndani  na Jukwaa la Wahiri Tanzania (TEF) katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Nimetoa maelekezo Nida, vitambulisho vilivyofutika vikusanywe haraka kutoka kwa wananchi vizalishwe upya, wapewe kwa sababu vitambulisho hivi ni muhimu na ndiyo kila kitu kwa sasa,” amesema Bashungwa.

Amesema vitambulisho hivyo vitazalishwa upya na kwa wakati na vitagawiwa upya bila mtu kutozwa gharama yoyote.

Wakati huohuo, Bashungwa amepongeza kasi ya utendaji wa Nida kuwa baada ya maagizo yake, ndani ya kipindi kifupi mamlaka hiyo imegawa vitambulisho 400,000 kwa wananchi ambavyo ni kati ya vitambulisho milioni 1.2 vilivyokuwa vimekaa ofisini kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa ametaja mikakati sita ya Serikali itakayoboresha na kuimarisha utendaji wa wizara hiyo pamoja na taasisi zake.

Mikakati hiyo inahusu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Dhumuni la mikakati amesema ni kupunguza na ikiwezekana kumaliza ajali za barabarani zinazogharimu maisha ya Watanzania.

Pia kupambana na majanga ya moto kwa kuongeza vitendea kazi, pamoja na kupata vitambulisho vya taifa kwa wakati. 

“Katika mikakati hii tumekusudia kuendeleza kampeni mbalimbali kama usalimishaji silaha kwa hiyari katika kipindi cha msamaha kinachotolewa kwa mujibu wa sheria, kuhamasisha jamii kuwakubali wafungwa walioachiwa kwa msamaha wa Rais, kampeni ya usalama wa barabarani,” amesema.

Amesema kampeni ya tahadhari ya kinga na moto na ile ya kutokukubaliana na wahamiaji haramu lengo ni kuwashirikisha wananchi kupitia kampeni ya ‘Mjue Jirani Yako.’

“Kampeni ya kuwarejesha wakimbizi kwa hiyari kwenye nchi zao, kuelimisha jamii juu ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na kuhamasisha jumuiya ya kijamii kufuata sheria za usajili. Kampeni zote hizi zitatekelezwa kwa miaka miwili ili kutengeneza msingi,” amesema Waziri Bashungwa.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Akitaja mikakati kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bashungwa amesema tayari magari mapya 12 yenye ubora yamepokewa na Jeshi hilo tayari kwa ajili ya kupambana na majanga ya moto nchini.

“Sambamba na hilo, habari njema kwa sasa tupo kwenye mchakato wa manunuzi ya magari mengine yenye ubora takribani 150, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani” amesema Waziri Bashungwa.

Katika kuboresha utendaji kazi, amesema wanafanya mazungumzo na Ofisi ya Rais Tamisemi katika suala la mipango miji izingatie miundombinu ya uzimaji moto.

“Tunazidi kujipanga na tunaongea na Tamisemi kwenye eneo la mipango miji, ujenzi wa ofisi na nyumba za makazi lazima ziendane sambamba na kuweka miundombinu ya maji ili litakapotokea janga la moto liweze kutatuliwa kwa haraka kwa sababu kuna miundombinu ya maji,” amebainisha.

 Kuhusu jinamizi la ajali

Waziri Bashungwa amesema lengo la Serikali ni kupunguza na kumaliza ajali za barabarani huku akibanisha kwamba tayari wameshakaa na Jeshi la Polisi kuangalia changamoto zilizopo ikiwemo katika mfumo wa utoaji leseni za udereva.

Ikumbukwe Desemba 31, 2024 akitoa takwimu za ajali kwa mwaka 2024, Rais Samia alisema takribani watu 1,715 wamepoteza maisha yao kwa ajali za barabarani huku wengine 2,719 wakijeruhiwa.

“Nilikaa na IGP, (Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini) na Latra (Mamlaka ya Udhibiti usafiir Ardhini) kujadili mfumo wa utoaji leseni kama upo madhubuti kiasi gani, vigezo na masharti vinavyotakiwa na kuna timu inaendelea kuchambua na kutekeleza yale tuliyokubaliana. Pale tunapopata wazembe tunaomba wawe mfano kwa wengine isifikie mtu ukiwa barabarani maisha yako yawe lehani,” amesema Bashungwa.

Hivyo, amewaomba wahariri na waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii namna ya kupambana na ajali za barabarani na kuwahamasisha kujiandikisha na kuchukua vitambulisho vyao vya Nida.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ametaja umuhimu wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu ya Serikali huku akisema kinachohitajika ni ushirikiano kati ya Wizara hiyo hasa upande wa Jeshi la Polisi na vyombo vya habari.

“Tunaomba IGP akutane na vyombo vya habari na Wahariri kama ilivyokuwa katika miaka ya 2000, vitakavyosaidia kufanikisha kazi za kiandishi na Jeshi la Polisi,” amesema Balile.

Related Posts