Mwanza. Tabia ya baadhi ya watumishi kugeuka madalali kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali maeneo mbalimbali nchini, imetajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vya ukusanyaji wa kodi na mapato katika miradi hiyo.
Miradi inayolenga kuongeza mapato, kama vile stendi ya mabasi, masoko na maeneo ya biashara, imekuwa haina ufanisi kutokana na changamoto hiyo, na hivyo kusababisha Serikali kupoteza mapato.
Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Januari 13, 2025, na Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Mwanza, Hamis Mjeye, ambaye amesema kuwa tabia ya watumishi wa Serikali kujimegea maeneo ya biashara kwenye miradi ya Serikali kisha kuvikodisha kwa wafanyabiashara kwa gharama kubwa, inasababisha Serikali kupoteza mapato ambayo yangepaswa kuingia serikalini.
Mjeye ametoa kauli hiyo alipozungumza katika kikao cha kwanza cha Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, kilicholenga kupokea maoni, changamoto na mapendekezo ya wafanyabiashara na wadau wa kodi nchini kutoka Mkoa wa Mwanza.
“Kwa nini hakuna walipa kodi wapya nchini? Hii ni kwa sababu vyumba vya biashara kwenye miradi hii ni vya watumishi wa Serikali. Maduka machache ndiyo yanayofanya kazi, lakini wanachukua vyumba vya biashara na kuviuza kwa bei kubwa, jambo ambalo linawafanya wafanyabiashara kuwa na ugumu kulipa kodi,” amesema Mjeye.
Amesema kuwa hali hiyo inasababisha upungufu wa mapato, na kwamba tatizo hili si la mkoa wa Mwanza pekee, bali ni janga la kitaifa. “Soko kuu limejengwa, lakini kuna fukuto kubwa; sisi hatukatai kodi, tunataka tulipe kodi rafiki, yenye uwazi na haki,” ameongeza Mjeye.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Chacha, amesema kuwa wafanyabiashara wameendelea kukumbwa na changamoto ya kukosa utaratibu wa kuchangia kulingana na uwezo wao, kutokana na kukithiri kwa utiriri wa kodi.
“Serikali inapaswa kutengeneza mfumo utakaomwezesha mfanyabiashara kulipa kodi zote kwa pamoja. Mfanyabiashara apate fursa ya kulipa kodi zote kwa wakati mmoja, na kuondoa usumbufu wa kila taasisi kutaka kumfikia mfanyabiashara,” amesema Chacha.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Hoteli jijini Mwanza, Nyiriza Makongoro, pia ameeleza kuwa sekta hiyo inakutana na utitiri wa kodi takribani 22. Ameshauri Serikali kupunguza kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi 15, na ushuru wa huduma (service levy) kutoka asilimia 0.3 hadi asilimia 0.1, ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa ushuru huo kwa urahisi.
“Kutokana na utitiri wa kodi, wafanyabiashara wanatafuta mianya ya kukwepa kodi au wanakutana na usumbufu mkubwa,” amesema Makongoro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa maoni na malalamiko yao yamepokelewa na yatashughulikiwa.
Balozi Sefue amesema kuwa lengo la kukusanya maoni hayo ni kuongeza idadi ya walipa kodi nchini na kuongeza mapato yatokanayo na kodi kutoka asilimia 12 ya sasa hadi asilimia 16 ya pato la Taifa.
“Watu wengi wanalalamikia faini za kuchelewa kulipa kodi, mlolongo mrefu wa ulipaji, na utitiri wa kodi. Tunatakiwa kuhakikisha kuna usawa wa ulipaji kodi, kwani mfumo ulivyo sasa hauwarahisishii wafanyabiashara, hasa wasiokuwa kwenye mfumo rasmi, kulipa kodi,” amesema Balozi Sefue.