Bodi ya Korosho kutumia BBT kufikia malengo

Lindi. Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeendesha mafunzo kwa vijana na maofisa kilimo 150 kutoka Mkoa wa Lindi kupitia programu ya “Jenga Kesho Ilio Bora” (BBT), lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa korosho nchini ili kufikia malengo ya Serikali ya kuzalisha tani milioni moja ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 13, 2025, Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Lindi, Ramadhani Khatibu, amesema Bodi ya Korosho imeamua kutoa mafunzo hayo kwa vijana ili kuboresha utendaji wao katika kusimamia pembejeo, viuatilifu, na kufufua mashamba pori kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa korosho.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa maofisa kilimo katika kuboresha usimamizi wa pembejeo, viuatilifu na kuhamasisha wakulima kufufua mashamba pori ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho,” amesema Khatibu.

Mwakilishi kutoka Bodi ya Korosho, George Nyaga, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa korosho hadi kufikia tani milioni moja ifikapo 2030, ambapo kwa sasa uzalishaji wa korosho umefikia tani laki nne.

Ameongeza kuwa kupitia programu ya BBT, Bodi ya Korosho imewaajiri vijana 500 ambao ni wataalamu wa kilimo, na kuwapeleka kwenye mikoa inayozalisha korosho kwa wingi kama vile Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga.

Shukrani Kwere, mtaalamu wa kilimo kutoka mradi wa BBT, amesema kuwa atajitahidi kufanikisha malengo ya Serikali kwa kuongeza uzalishaji wa korosho kupitia usimamizi bora wa viuatilifu na pembejeo.

Joseph Mkude, Ofisa Kilimo kutoka Kilwa, ameeleza kuwa mafunzo hayo yatamsaidia kutoa msaada kwa wakulima kwa kuhakikisha wanapata pembejeo na viuatilifu bora, huku akiwashauri kufufua mashamba pori ili kuongeza idadi ya mikorosho na kufikia malengo ya Serikali.

Related Posts