Morogoro. Waziri wa Ujenzi, Abdalah Ulega, amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde, kuhakikisha eneo la Dakawa, lililopo wilayani Mvomero, linawekwa taa za barabarani na kujengwa maeneo ya maegesho ya magari ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao wakati wote.
Ulega ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 13, 2025 wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Morogoro, ambapo alisimama eneo hilo na kuzungumza na wananchi wakiwemo wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kando ya barabara.
Aidha, amemtaka Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, kuhakikisha anamaliza kazi hiyo haraka baada ya kupata fedha kutoka wizarani, na ameahidi kurudi kuzindua taa na maeneo ya maegesho punde ujenzi utakapokamilika.
Awali, Mhandisi Kyamba alitoa taarifa kwa Waziri Ulega amesema ujenzi wa taa na maegesho katika eneo hilo utagharimu Sh300 milioni. Ameongeza kuwa, taa 50 zitakazowekwa na ujenzi wa eneo la maegesho yenye urefu wa mita 200 zitatosha kuhudumia magari yatakayokuwa yakiegeshwa katika eneo hilo.
Msonde ameahidi kutekeleza agizo hilo la kuweka taa za barabarani katika eneo hilo la Dakawa, huku akimtoa wasiwasi Waziri Ulega kuwa fedha za kuweka taa hizo zitapatikana.
Wakati akiwa katika Manispaa ya Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, alimuomba Waziri Ulega kuangalia uwezekano wa kuweka taa katikati ya mji, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuifanya Manispaa hiyo kuwa Jiji.
Kilakala amesema maeneo mengi ya mji huo yapo giza usiku, jambo linaloleta hatari kwa usalama wa wananchi.
Kilakala ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka zaidi ya Sh134 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki, ambayo itachochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Wananchi wa Dakawa wameeleza kuridhishwa na hatua ya Serikali kuweka taa katika eneo hilo, wakisema kuwa hatua hiyo itachangia kufanya eneo hilo kuwa na shughuli za kibiashara za usiku.
Joseph Eliabi, mmoja wa wananchi, amesema kuwepo kwa taa kutawasaidia kuchangamkia fursa za kibiashara hasa katika biashara za kuchoma mahindi na nyingine zinazofanyika usiku.