TIMU ya Taifa ya Zanzibar Heroes, imefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2025 baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 2-1.
Katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Januari 13, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, Zanzibar Heroes ilikuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 41 kupitia mshambuliaji Ibrahim Hamad Hilika.
Hilika alifunga bao hilo kiufundi kwa kisigino baada ya kupokea pasi kutoka kwa Salum Khamis Gado. Zanzibar Heroes ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, Burkina Faso walikuja na mpango tofauti wakiongeza mashambulizi zaidi langoni mwa Zanzibar Heroes wakafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 70 kupitia kwa Aboubacar Traore.
Traore ambaye hilo ni bao lake la pili katika mashindano hayo, alilifunga kwa shuti kali akiwa nje ya boksi la Zanzibar Heroes lililomshinda kipa Yakoub Suleiman.
Ule msemo wa haijaisha mpaka iishe, ulidhihirishwa na Zanzibar Heroes ambapo shambulizi la mwisho dakika ya 90+2 walilitumia vizuri kufunga bao la ushindi kupitia Hassan Ali ‘Cheda’.
Cheda alitumia vizuri mpira uliookolewa na beki wa Burkina Faso baada ya nahodha wa Zanzibar Heroes, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kupiga kona, akafunga bao hilo ambalo liliibua shangwe kubwa Uwanja wa Gombani.
Kipigo hicho kimekuwa cha kwanza kwa Burkina Faso katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kushinda mbili na sare moja hatua za mwanzoni, lakini pia Zanzibar Heroes ni kama imelipa kisasi baada ya kufungwa 1-0 na Burkina Faso katika mchezo wa pili.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, zilitolewa zawadi kwa wachezaji waliofanya vizuri katika michuano hiyo ambapo nyota wa Kilimanjaro Stars, Abdulkarim Kiswanya alitajwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi.
Tuzo ya Kipa Bora imekwenda kwa Yakoub Suleiman wa Zanzibar Heroes, Mchezaji Bora ni Clement Pitroipa (Burkina Faso) wakati Mfungaji Bora ni Aboubacar Traore (Burkina Faso) akimaliza na mabao mawili.
Mabingwa Zanzibar Heroes walikabidhiwa shilingi milioni 100 na kombe.
Michuano hiyo iliyoanza Januari 3 na tamati yake kuwa Januari 13 mwaka huu ikifanyika Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba, ilishirikisha timu nne ambazo ni Kilimanjaro Stars, Kenya, Burkina Faso na wenyeji Zanzibar Heroes.