Hiki hapa kinachozibeba Simba, Yanga Caf

SIMBA juzi ilitinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Bravos ya Angola huku Yanga ikijiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Al Hilal huko Mauritania.

Kwa sasa, Yanga inahitaji ushindi tu katika mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya MC Alger, Jumamosi hii ili ifikishe pointi 10 na kutinga robo fainali wakati Simba inahitaji ushindi katika mechi yake ya mwisho nyumbani dhidi ya CS Constantine ya Algeria iweze kuongoza kundi.

Kama zote zikifanikiwa kutinga robo fainali, mabenchi yao ya ufundi yatakuwa na uhakika wa kuwatumia wachezaji wao wote iwapo hawatakuwa majeruhi kwa vile hakuna hata mmoja kati yao ambaye amekusanya idadi ya kadi za njano ambazo zitamuweka katika hatari ya kukosa robo fainali ikiwa ataonyeshwa kadi ya njano kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi mwishoni mwa wiki hii.

Ibara mbili za kanuni za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zimeirahisishia kazi Simba katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na hata Yanga iwapo itafanikiwa kutinga hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ibara zote hizo ni za kanuni ya tano ambayo inafafanua hatua za kinidhamu ambazo zinachukuliwa kwa wachezaji katika mashindano ya klabu Afrika.

Kwa mujibu wa ibara ya kwanza, mchezaji akionyeshwa kadi tatu za njano, anakosa mchezo unaofuata wa ama Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika.

“Mchezaji anayetimiza kadi tatu za njano, anasimamishwa moja kwa moja kucheza mchezo unaofuata wa mashindano ya klabu ya Caf. Kusimamishwa huko kunatakiwa kutolewe taarifa na sekretarieti kwenda kwa vyama husika.”

Hata hivyo, ibara ya tatu Ligi ya Mabingwa Afrika inafafanua kuwa mchezaji ambaye hajapata idadi ya kadi zinazomfanya akose mchezo katika hatua ya makundi, pindi inapomalizika kadi hizo haziendelei kuwa hai.

Hadi zinaingia katika raundi ya mwisho ya hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, Simba na Yanga kila moja haina mchezaji anayeweza kutimiza idadi ya kadi tatu za njano.

Katika mechi tano za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ina kadi tano tu za njano ambazo zimeonyeshwa kwa Leonel Ateba, Mousa Camara, Che Fondoh Malone, Debora Fernandes na Kibu Denis.

Ni kama ilivyo kwa Yanga ambayo nayo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ina kadi tano za njano zilizoonyeshwa kwa wachezaji Djigui Diarra, Clatous Chama, Ibrahim Hamad, Kibwana Shomari na Pacome Zouzoua.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inaongoza kwa kupata kadi chache ikiwa nazo tano ambazo zote ni za njano na kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba inashika nafasi ya pili kwa kupata idadi ndogo ya kadi hizo, inazo tano.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Pwani (Corefa), Robert Munisi alisema maandalizi mazuri ya kinidhamu ambayo Yanga na Simba zimeyapata nyumbani yamechangia kuzipa heshima kimataifa.

“Huwezi kufika hapo kama hauna nidhamu. Na nidhamu sio ya uwanjani tu bali hata nje ya uwanja. Sasa Simba na Yanga zimeonyesha hilo na ndio maana unaona mapema Simba imefuzu na Yanga ipo katika nafasi nzuri.

“Lakini pia nipongeze Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kwa kusimamia vyema nidhamu katika ligi yetu jambo ambalo linafanya timu zetu kuihamishia kimataifa kama hivi tunavyoona,” alisema Munisi.

Related Posts