Dar es Salaam. Wajumbe wa Baraza la Wazee (Bazecha) wamemchagua Suzan Lyimo kuwa mwenyekiti mpya wa baraza hilo kwa miaka mitano ijayo baada ya kujinyakulia kura 96 huku nafasi ya katibu mkuu akishinda Hellen Kayanza.
Lyimo ametangazwa mshindi baada ya kuwabwaga wapinzani wake wanne akiwamo Hashim Issa aliyepata kura 14 aliyekuwa akitetea nafasi hiyo aliyohudumu kwa miaka 10.
Wengine waliobwagwa na Susan ambaye katika uongozi uliopita alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bazecha, Tanzania bara ni Hugo Kimaryo aliyepata kura 5, John Mwambigija (23) na Merchard Tiba (5).
Suzan anakuwa mwanamke wa kwanza kuhudumu katika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa baraza hilo.
Kwa upande wa nafasi ya katibu mkuu imetangazwa kunyakuliwa na Hellen Kayanza kwa kura 115.
Awali, Hellen alikuwa akitumikia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu Tanzania bara.
Hellen amewabwaga washindani wake watatu, walioingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo, akiwamo Casmir Mabina aliyepata kura 10 na Leonard Mao kura 13.
Nafasi ya makamu mwenyekiti Tanzania Bara, ametangazwa Shaban Madede aliyepata kura 123 na alikuwa mgombea pekee aliyepigiwa kura ya hapana na ndiyo.
Pia, nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar, Hamoud Mohammed ametangazwa kushinda kwa kura 105 dhidi ya Mohammed Haji aliyepata kura 33.
Katika nafasi ya naibu katibu mkuu Tanzania Bara, mshindi ni Hamida Mfaligunda aliyepata kura 103 huku mshindani wake wa Omary Mkama akipata kura 30.
Naibu katibu mkuu Zanzibar ni Rajab Bakari aliyepata kura 117.
Idadi ya wajumbe hadi matokeo yanatangazwa ilikuwa pungufu ikilinganishwa na waliojitokeza kupiga kura jana.
Upungufu huo ulichochewa na wajumbe kulala ndani na nje ya ukumbi lakini wengine wakionekana kuwa jino kwa jino na viongozi waliosimamia uchaguzi huo kuhakikisha hakuna wizi wa kura.
Baada ya sauti ya mwenyekiti kusikika akisema shughuli ya kuhesabu kura imetamatika na ni wasaa wa kutoa matokeo, wajumbe waliingia ndani kutangaziwa na kupewa zawadi.
Zawadi hiyo ni kofia ikiwa ni shukrani ya uvumilivu wao tangu shughuli waliyoianza jana asubuhi hadi leo Januari 14 walipotangaziwa safu mpya ya uongozi waliyoichagua.
Ilikuwa ni nafasi yao ya kipekee kwa wajumbe hao kukutana kwa awamu ya pili huku wakinong’onezana na wengine wakishikana mikono kupiga picha za pamoja kama ishara ya furaha kwa kazi waliyoifanya.
Baada ya ushindi huo, Suzan amewashukuru wajumbe waliothubutu kugombea nafasi mbalimbali huku akiwataka kila mmoja kutambua wajibu wake.
“Kamwe tusiwe chanzo cha chokochoko bali tusimame katika kama wapatanishi,” amesema Susan.
Amesema baada ya kuona vipaji vya wagombea mbalimbali wakati wanajinadi ameahidi kutoa fursa kwa wenye ujuzi ili wachaguliwe kulitumikia baraza hilo.
Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa Bazecha, Eliakim Maki amelazimika kupiga kura ya turufu kuamua anayepaswa kuwa mjumbe wa baraza katika mkutano mkuu kwa Tanzania bara.
Msingi wa kupigwa kura hiyo ni baada ya wajumbe watatu kulingana kura walipata 47 na ilitakiwa apatikane mmoja ili kutimiza idadi ya wajumbe 15 wanaotakiwa.