Prisons yabadili gia kwa Sabato

TAARIFA zinabainisha Tanzania Prisons imeachana na mpango wa kuendelea na mshambuliaji Kelvin Sabato, badala yake inapambana kusaka mrithi wake huku jina la Yusuph Athuman likitajwa.

Awali Prisons ilimpa Sabato mkataba wa miezi sita kipindi hiki cha usajili wa dirisha unaofungwa leo Jumatano, lakini baadaye ikaamua kuchana naye huku sababu kubwa ikitajwa ni nidhamu.

Imeelezwa kati ya usajili alioukubali kocha mpya wa timu hiyo, Aman Josiah mwenye Leseni A ya CAF ni wa mshambuliaji Adam Adam aliyetokea Azam FC kwa mkopo na sasa anahitaji ipatikane saini ya Athuman.

Hata hivyo, ishu ya kumpata Athuman inaweza kuwa ngumu kwani mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amejiunga na Fountain Gate kipindi hiki cha dirisha dogo.

“Kutokana na nafasi iliyopo timu yetu na tunaingia mzunguko wa pili ambao utaamua kila kitu ikiwemo bingwa na timu zipi zitashuka, tumeona tunahitaji kupata wachezaji wazuri ambao watatusaidia kufikia malengo yetu na si vinginevyo.

“Kocha amefurahishwa na usajili wa Adam Adam na anahitaji asajiliwe Athuman, viongozi wapo mbioni kulikamilisha hilo,” kilisema chanzo.

Katika kuendelea kujiimarisha, pia Prisons imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Gustavo Simon kwa mkataba wa miezi sita kutoka Dodoma Jiji, kilichobaki ni kutambulishwa.

Related Posts