Fei Toto ataja kilichowabeba Mapinduzi Cup

NAHODHA wa kikosi cha Zanzibar Heroes, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefichua kujituma kwao mwanzo hadi mwisho ndiyo siri kubwa ya kuwa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi 2025.

Zanzibar Heroes ilibeba ubingwa wa michuano hiyo baada ya jana Jumatatu kuichapa Burkina Faso mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba.

Katika mchezo huo wa fainali, Zanzibar ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 41 lililifungwa na Ibrahim Hamad Hilika, Burkina Faso ikasawazisha dakika 70 mfungaji akiwa Aboubacar Traore kabla ya Hassan Ali ‘Cheda’ kuifungia Zanzibar bao la ushindi dakika ya 90+2.

“Michuano ilikuwa migumu lakini juhudi zetu na kujituma uwanjani zilitufanya tubebe ubingwa wa mashindano haya,” alisema Fei Toto.

Kwa upande wa Kocha wa Zanzibar Heroes, Ali Bakar Ngazija amewasifu wachezaji wake akiwemo Fei Toto aliyekuwa na mchango mkubwa katika michuano hiyo akifunga bao moja waliposhinda 1-0 dhidi ya Kilimanjaro Stars.

“Fei ni mchezaji mzuri anayejielewa na kubarikiwa kipaji, naamini kwa mwenendo huo anaweza kufika mbali,” alisema kocha Ngazija.

Zanzibar Heroes katika michuano hiyo ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kilimanjaro Stars mfungaji akiwa Fei Toto.

Kisha wakafungwa 1-0 na Burkina Faso, kabla ya kuichapa Kenya 1-0 na kutinga fainali ikienda kulipiza kisasi kwa Burkina Faso ikiichapa mabao 2-1.

Fei Toto mbali na kufunga bao moja, pia alitoa asisti ya bao lililofungwa na Ali Khatib ‘Inzaghi’ katika mchezo dhidi ya Kenya na ushindi huo uliwafikisha fainali.

Pia mchezo wa fainali, kona aliyopiga ndiyo ilizaa bao la ushindi na kubeba kombe.

Related Posts