Mgogoro wa shamba Mbarali waua wawili, watatu mbaroni kwa mauaji

Mbeya. Wakazi wa Igurusi wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Wilbroad Mjengwa (38) na Maige Jirafu (44) wameauawa katika mgogoro wa kugombea shamba. Tayari Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayo. Tukio hilo limedaiwa kufaywa na kundi la watu zaidi ya 15 ambapo mbali na kufanya mauaji hayo, pia walijeruhi wengine watano kwa kutumia silaha mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameliambia Mwananchi leo Jumanne Januari 14,2025 kuwa tukio hilo limetokea Januari 10, 2025 saa 10.00 jioni katika Kijiji cha  Shitanda Kata ya Luhanga wilayani humo.

Imeelezwa kuwa wakati tukio hilo likitokea familia ya watu waliopoteza maisha walikuwa kwenye maandalizi ya shamba hilo lenye mgogoro ambalo wana hati miliki.

Kamanda Kuzaga amesema awali kulizuka ugomvi baina ya familia mbili ya Raphael Mjengwa mmiliki halali wa shamba lenye ukubwa wa hekari 1,050 mwenye hati miliki iliyotolewa mwaka 1987, dhidi ya familia ya Mzee Malewa ambao, walidai eneo hilo walikuwa wakilitumia kwa kilimo na kulisha mifugo.

“Siku ya tukio familia ya Mlewa walikuwa kwenye maandalizi ya msimu wa kilimo katika shamba hilo lenye mgogoro,” amesema na kuongeza”

Ghafla wakiendelea na maandalizi walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 15 ambao walianza  kuwashambulia kwa silaha mbalimbali na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine watano kujeruhiwa.”

Kuzaga amesema kufuatia tukio hilo, Polisi walianza msako na jana Januari 13,2025 usiku  katika Kata ya Luhanga waliwatia mbaroni watu watatu ambao ni miongoni mwa waliohusika na tukio hilo.

Related Posts