Profesa Juma : Tutaadhimisha Wiki Ya Sheria Kwa Kutoa Elimu Kwa Umma

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

KATIKA kukuza uelewa wa mifumo ya utoaji haki pamoja na haki madai mahakama nchini imesema kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan katika kuadhimisha wiki ya sheria nchini.

Hayo yamesemwa leo Januari 14, 2025 na Jaji Mkuu nchini Profesa Ibrahim Juma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na wiki ya sheria na siku ya sheria itakayoanza Januari 25 hadi Februari Mosi, 2025, siku ya sheria itafanyika Februari 3, mwaka huu mgeni rasmi ni Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Profesa Juma amesema wananchi wengi bado wanaogopa Mahakama, hawatakiwi kuogopa kwa sababu haki inapatikana huko pamoja na maridhiano ndiyo maana wanaendelea kuwasogezea huduma za Mahakama karibu.

Amesema katika kuadhimisha wiki ya sheria kwa mwaka huu watatembelea Shule za msingi, Sekondari, vyuoni na kwenye mikusanyiko ya watu kwa lengo la kutoa elimu kuhusu haki madai na pia kuwaeleza shughuli zinazofanywa na Mahakama.

Amesema kwa kuzingatia kwamba maadhimisho hayo yanafanyika siku za kazi ambazo wananchi wengi wanakuwa kwenye shughuli zao za kutafuta kipato katika utoaji wa elimu mwaka huu tutajaribu kuwafuata wananchi pale walipo.

“Tutaenda kwenye maeneo ya makazi tofauti na ilivyokuwa awali tulikuwa tunategemea wananchi watufuate katika maeneo ambayo tumetenga, tutatoa elimu katika masuala mbalimbali ya kisheria kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu,”

“Tutatumia magari maalumu yatakayokuwa yanahama kutoka eneo moja kwenda lingine na lengo ni kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa umma, pia tutatembelea shule za msingi, sekondari na vyuo, ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi wafahamu shughuli za Mahakama,”amesema Profesa Juma

Profesa Juma amesema kuanzia mwaka 2015 wamekuwa wakifanya maboresho katika utoaji haki na wameweza kutumia mpango mkakati na programu za maboresho ambazo zimewasaidia kufanya maboresho ambayo yanaonekana.

“Maboresho haya yamekuwa yakiongozwa na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, kwa hiyo tunaweza kusema sisi tunauzoefu wa kuweza kujitayaarisha tufanye nini na tufanye mageuzi gani ili tuweze kusaidia taifa letu wakati wa utekeleza wa dira ya mwaka 2050,”

“Hii wiki ya sheria inaumuhimu mkubwa sana, umuhimu wa kumaliza dira iliyopita na kujitayarisha na dira mpya ambayo imeongeza matumaini kwa watanzania, sisi tunaogopa kwamba tusipojitayarisha katika mfumo mzima wa utoaji haki madai tusionekane sisi ndiyo tatizo, sisi ndiyo kikwazo cha mafanikio ambayo yametajwa kwenye rasimu ya dira,”amesema.

Amesema kwa mwaka huu utoaji elimu utahusisha majaji, wasajili, watendaji wa Mahakama na pia watashirikiana na wadau wengine muhimu na taasisi zingine zilizokuwepo katika mfumo wa haki jinai ili wananchi waweze kuweza kujifunza na kuuuliza maswali.

Aidha amesema kuwa wanasoma yote yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari na mambo yoyote yaliyoibuliwa ambayo ni mapungu kwao wanayafanyia kazi, chochote kinachosemwa na kuandikwa hata kama sio kizuri huwa wanakifanyia kazi na hata tuhuma pia wanazifanyia kazi.

“Tunapenda kuwarudia wananchi kila baada ya miaka mitatu kupitia taasisi isiyokuwa ya kiserikali REPOA huwa inafanya utafiti kwa kuwauliza wananchi maeneo gani ya huduma yetu ambayo inawaridhisha na ambayo hayawaridhishi,”

“Naomba mara kwa mara muwe mnasoma taarifa za utafiti kuhusu mahakama taarifa hii ya REPOA inaainisha mapungufu yetu mengi tu kwa sababu tunakaribisha mapungufu, tunapombana nayo maana yake ni maboresho usipoletewa mapungufu huwezi kufanya maboresho,”amesema

Amesema mgeni rasmi katika uzinduzi wa siku ya sheria Kitaifa, itakayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Square jijini Dodoma Januari 25,2025 anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete
 

JAJI Mkuu Nchini, Profesa Ibrahim Juma akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea siku ya Sheria Februari.Nchini itakayofanyika Februari  3, 2025 ambayo itatanguliwa na wiki ya sheria kuanzia Januari 25 na kumalizika Februari Mosi Mwaka huu ambapo Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Related Posts