Chungu na tamu ongezeko la maji Ziwa Victoria, Tanganyika

Mwanza/Muleba. Athari za ongezeko la maji Ziwa Victoria na Tanganyika zinazidi kuonekana kila kukicha.

Hii ni baada ya wavuvi zaidi ya 100,000 mkoani Kigoma kudaiwa kuathirika na ongezeko hilo huku kaya 214 za Muleba Mkoa wa Kagera zikikosa vyoo.

Pia gharama za kupakia na kushusha mizigo katika soko la kimataifa la samaki mwalo wa Kirumba jijini Mwanza nako wakiongeza tozo kutoka Sh1,000 na kufikia Sh3,000 kwa gunia moja.

Katibu wa wavuvi mkoani Kigoma, Bakari Almasi akizungumza na Mwananchi Digital amesema wavuvi waliokuwa wakiishi pwani ya Ziwa Tanganyika, wamelazimika kuhama maeneo yao baada ya maji kujaa.

Amesema Mei 15, 2024, shughuli za uvuvi zitafungwa kwenye ziwa hilo kwa miezi mitatu na watu hao hawajui mustakabali wa maisha yao mpaka sasa.

“Hali ya wavuvi ni ngumu, wamelazimika kuhama makazi yao baada ya kujaa maji…mfano mwalo wa Kibirizi wote sambamba na soko la kuuzia samaki na dagaa limejaa maji, kuna mwalo mkubwa pale Ujiji wa Forodhani nao umejaa maji watu wamehama, kuna mwalo wa Mgambo wilayani Uvinza pia umejaa maji watu wamehama, mwalo wa Kigwesa na wa Kabeda yote watu wameihama baada ya kujaa maji,” amesema Almasi.

Amesema hali hiyo inaathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.

“Sisi huku tuna eneo tunaloliita mbuga, ni sehemu ya wazi zinapoanikwa dagaa, nalo limemezwa na maji lakini pia kuna maeneo ya makazi ambayo watu walikuwa wameweka kambi nayo pia yamechukuliwa na maji, Kwa hiyo gharama zote hizo zinakwenda kuwaumiza wavuvi,” amesema  Almasi.

Anasema mpaka sasa inakadiriwa kambi 26 kwenye visiwa vya uvuvi zimeathiriwa kati ya visiwa 58 vilivyopo ziwani humo.

Inaelezwa jumla ya kaya  214 zinazoishi kwenye visiwa vitano Wilaya ya Muleba mkoani Kagera hazina vyoo baada ya maji kuongezeka na kuvibomoa.

Ofisa Afya na Mazingira wilayani humo, Johanes Mutoka amesema wananchi wa visiwa vya Bumbile, Ikuza, Kerebe, Mazinga na Goziba wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Johanes amesema wilaya ya Muleba inaundwa na kata 43 na tano zipo visiwani na zina wakazi wa kudumu 53,832 huku visiwa vyote ndani ya ziwa Victoria kwa upande wa wilaya hiyo vikiwa 39 kati ya hivyo, 25 ndio vyenye makazi ya watu.

“Wilaya yetu ina changamoto ya baadhi ya wananchi kutokuwa na vyoo salama kwa sababu takwimu zinaonyesha asilimia 75 ndiyo wenye vyoo bora na asilimia 25 wanatumia vya asili ambavyo si salama na zaidi ya kaya 214 hazina vyoo kabisa,” amesema.

Kutokana na tatizo hilo, Johanes ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari ya kujenga vyoo na kutumia maji yaliyotibiwa ili kuepukana magonjwa ya mlipuko.

Amesema adha ya kujaa maji ilishakikumba kisiwa cha Goziba mwaka jana ambako  kipindupindu kililipuka na kusababisha watu sita kufariki dunia.

Kisiwa hicho kinachosifika kwa uvuvi wa dagaa na samaki, ni kati ya visiwa vinavyokaliwa na watu wengi na takwimu za Januari hadi Machi, mwaka huu zinaonyesha kina kaya 2,988, wakazi 11,056 na kati ya hao, wanatumia vyoo vya asili wako 235 na vyoo  salama 2,736.

Mkazi wa kisiwa hicho, Grace Joseph ambaye ni muhudumu wa nyumba za kulala wageni amesema eneo analofanyia kazi, nyumba zote zimejaa maji kutoka Ziwa Victoria yaliyobomoa vyoo vingi na ameiomba Serikali kuwasaidia ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na kunusuru makazi yao.

Maji yapaisha bei ya kubeba mizigo Mwanza

Mfanyabiashara katika Soko la Kimataifa la Samaki la Kirumba Mwaloni, Frank Batholomeo akizungumzia bei ya samaki, amesema kuongezeka kwa maji kumesababisha ongezeko la gharama za kushusha na kubeba mizigo sokoni hapo.

Amesema hivi sasa wanalazimika kulipia gunia moja la bidhaa Sh3,000 kutoka Sh1,000 ya awali.

“Hapa tunategemea biashara hii, sasa unatumia gharama kubwa kuagiza mzigo kisiwani unaleta hapa napo pia unatumia gharama kushusha sisi kwetu tunapata hasara ukizingatia tunalipa pia ushuru. Serikali itusaidie kuinua daraja (ghati) hili lipo chini sana, likiendelea kubaki hivi  tutaendelea kuingia hasara mwishowe tutaishiwa mitaji,” amesema Batholomeo. 

Naye mfanyabiashara wa dagaa mwaloni hapo, Helena Gibole amesema mbali na gharama ya kushusha mizigo kuongezeka pia mitumbwi mingi imepasuka, ikibeba mizigo mingine hutumbukia ziwani hasa inapopakuliwa kutoka kwenye boti ili ifikishwe nchi kavu.

“Tulikuwa tunashushia mzigo kwa Sh500 lakini saizi imepanda mpaka Sh1,000 muda mwingine mizigo inadondoka kwenye maji inakuwa changamoto kuanika, lakini pia soko letu mvua kubwa ikiwa inanyesha linavuja, kifupi hatuko salama,” amesema Gibole.

Mfanyabiashara wa vinywaji katika soko hilo, Mussa Lukantanga ameomba viongozi wa soko hilo kuwatafutia eneo lingine la biashara katika kipindi hiki ambacho maji yameongezeka ziwani. 

“Ongezeko la maji kwangu limenibania sana riziki, huko nyuma nilikuwa na uhakika wa kuuza kuanzia Sh100,000 mpaka Sh180,000 lakini sasa nauza wastani wa Sh10,000 kwa siku kwa sababu ongezeko la maji limefanya wateja nao wapungue sokoni hapa,” anasema Lukantanga.

Wengine watumia kama fursa

Baadhi ya vijana wa mwalo wa Kirumba wamechukulia kuongezeka huko kwa maji ziwani ni fursa kwao kama walivyokutwa na Mwananchi Digital.

Vijana hao wamegeuza changamoto hiyo kuwa fursa baada ya kujiingizia kipato kupitia kuvusha watu na mizigo kwa matolori. 

Mmoja wa vijana hao ambaye pia ni mkazi wa Kitangiri, Olombe Nyawala amesema mbali na kukumbana na changamoto ya kuteleza na kuumia wakati wakifanya shughuli hiyo, wamekuwa wajiingizia kipato ambacho awali walikuwa hawakipati.

“Tunavusha mtu kwa Sh500, lakini akiwa na mzigo tunamtoza Sh1,000, kwangu mimi hii ni fursa kwa sababu ninaweza kuingiza kuanzia Sh5,000 na kuendelea kitu ambacho huko nyuma ilikuwa ngumu kukipata,” amesema Nyawala. 

Akiunga mkono hoja hiyo, Peter Bernad amesema anatamani maji yasipungue mapema ili wajiingizie kipato cha kutosha.

Lakini hali ni tofauti kwa Joseph Juvenali ambaye hubeba magunia ya dagaa mwaloni hapo ambaye ameiomba Serikali ijenge upya gati katika eneo hilo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

“Maji yanatusumbua sana, unakuta unatoka kule kwenye meli na gunia la dagaa, ukifika darajani unadondoka wakati huo huo linatakiwa lisafirishwe kwenda mikoani, sasa baada ya kudondoka inabidi muanze kuanika kitu ambacho ni changamoto na kama gari lilikuwa linataka kuondoka linatuacha,” amesema Juvenali.

Mwenyekiti wa Soko la Kimataifa la Samaki la Kirumba Mwaloni, Fikiri Magafu amesema tayari  wameifikisha adha hiyo kwa mamlaka husika na wataalamu wameshafika katika eneo hilo kwa ajili kulitafutia ufumbuzi. 

“Sehemu nyingi zimejaa maji na tunachofanya ni kuwahamisha wafanyabiashara na kuwapeleka katika maeneo ambayo hayana maji waendelee na biashara zao. Ukiangalia hata kule darajani nako kumemezwa na maji,” amesema.

Katika nyakati tofauti, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Gerald Itimbula na Mhandisi Odemba Ododa kutoka Bonde la Ziwa Tanganyika walisema kina cha maji kwenye maziwa hayo kimeongezeka.

Related Posts