SIMBA SC itacheza mechi yake ya Jumapili wiki hii Januari 19, 2025 dhidi ya CS Constantine bila ya mashabiki kufuatia adhabu iliyopewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Adhabu hiyo imekuja baada ya kutokea vurugu katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu dhidi ya CS Sfaxien uliofanyika Desemba 15, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-1, zilitokea vurugu ambazo zilisababisha viti 256 kuvunjwa.
Simba imethibitisha kupokea adhabu hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu, Zubeda Sakuru huku ikiabinisha kwamba awali walifungiwa mechi mbili lakini sasa imebaki moja ya mwisho kumaliza makundi.
Taarifa hiyo imesema: “Klabu ya Simba imepokea maamuzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) kuhusu vurugu zilizojitokeza katika mchezo wetu dhidi ya CS Sfaxien uliofanyika Disemba 15, 2024.
“Uamuzi huo wa CAF umeifungia klabu yetu mechi mbili, hata hivyo adhabu hiyo imepunguzwa kuwa mechi moja kucheza bila mashabiki pamoja na faini Dola elfu 40,000.
Hivyo tunapenda kuufahamisha umma kuwa tunaendelea kufanya taratibu ili kushughulikia uamuzi huo.
“Kwa maamuzi hayo klabu inasitisha mauzo ya tiketi ya mchezo wetu dhidi ya CS Constantine na kwa mashabiki ambao wameshanunua tiketi tunaomba tiketi hizo zitatumika kwenye mchezo ujao wa robo fainali.
“Klabu ya Simba itaendelea kusimamia taratibu, kanuni na sheria zinazozingatia usalama wa jumla katika michezo.”
Simba tayari imefuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo kuanzia hatua hiyo itaruhusiwa kuingiza mashabiki.