Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mwaka 2025 Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira yatakayohamasisha biashara na uwekezaji.
Amesema hayo leo Januari 14, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusherehekea Mwaka Mpya iliyowakutanisha mabalozi wa mataifa mbalimbali waliopo nchini.
Akitoa tathmini ya mwaka 2024, amesema ulikuwa wa kihistoria ambao pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 ya mwaka 2023.
Amesema katika uwekezaji, Tanzania ilivutia uwekezaji wenye thamani ya Dola 7.7 bilioni za Marekani mwaka 2024.
“Ukuaji huu umeonekana pia Zanzibar ambako tumeshuhudia zaidi ya miradi 160 ya uwekezaji iliyotengeneza ajira 3,376. Ukuaji wa uwekezaji huu unaashiria namna ambavyo mataifa yamekuwa na imani na Tanzania, hivyo tutaendelea kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji,” amesema.
Amesema mbali na kuongezeka kwa uwekezaji pia kumekuwa na maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwamo uuzaji wa bidhaa nje ya nchi ambao hadi kufikia Septemba 2024 thamani yake ilikuwa Dola 15 bilioni kutoka Dola 13.5 bilioni mwaka 2023.
Kwenye sekta ya utalii amesema kwa mwaka 2024 mapato yameongezeka kufikia Dola 3.6 bilioni kutoka Dola 3.4 bilioni mwaka 2023.
“Ukuaji huu umeenda kuchangia asilimia 17 ya pato ya Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni. Tunaahidi kuendelea kusimamia ukuaji wa sekta hii ili kufikia lengo letu la kupata watalii milioni tano kwa mwaka,” amesema.
Rais Samia amesema eneo lingine la kipaumbele ni kusimamia vyema mfumo wa kodi, akieleza mwaka 2024 Serikali iliunda kikosi kazi ambacho kimepewa jukumu la kuufanyia mapitio mfumo wa kodi na ripoti inatarajiwa kutoka Machi, mwaka huu.
Katika eneo la utawala Rais Samia amesema falsafa ya 4R imeendelea kuwa mwongozo wa Serikali ambayo imetengeneza mazingira yanayoruhusu majadiliano yanayolenga kuhamasisha umoja na mshikamano kwa faida ya Watanzania wote.
“Hili limetusaidia katika uchaguzi wa Serikali za mitaa (ulifanyika Novemba 27, 2024), amani na utulivu vilitawala na sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, tumejipanga kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria vinazingatiwa,” amesema.
Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Dk Ahamada El Badaoui akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, amesema wako tayari kuunga mkono jitihada zinazofanyika nchini.
Amezitaja jitihada hizo ni pamoja na mapambano dhidi ya ufisadi, kuboresha ustawi wa Watanzania kupitia maendeleo jumuishi, mapambano dhidi ya umaskini, kuboresha mfumo wa elimu na kuhakikisha watu wote wananufaika na utajiri na rasilimali za Tanzania.