Gamondi anusurika, waamuzi wafungiwa | Mwanaspoti

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amepishana na adhabu ya kifungo baada ya kupigwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kufanya vurugu ikiwemo kuwashambulia kwa maneno makali waamuzi wa mchezo dhidi ya Kagera Sugar adhabu iliyotolewa na Kamati ya Uendeshwaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi.

Adhabu hiyo itashusha presha kwa viongozi na mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wakisubiri kujua kipi kitamkuta kocha huyo kufuatia matukio hayo yaliyojiri mara baada ya mchezo huo kumalizika.

Hata hivyo, kamati hiyo imemfungia mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo huo, Shaban Mussa kutoka Geita na ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa kutafsiri vizuri sheria za mpira wa miguu baada ya kukataa bao halali la mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede akidai mfungaji kabla ya kufunga alikuwa ameotea.

Mwamuzi Frank Chavala kutoka Morogoro aliyekuwa mwamuzi wa kwanza msaidizi kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Tabora United naye amekumbana na adhabu kama hiyo baada ya kukataa bao la kiungo wa Tabora, Najim Mussa akidai mpira haukuvuka mstari.

Nayo klabu ya Geita Gold imetozwa faini faini ya Sh500,000 kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalumu cha kuvalia nguo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ilipocheza dhidi ya JKT Tanzania, Mei 4,2024, wakati meneja wa timu hiyo, Abeid Choke akifungiwa mechi tatu kwa kosa la kuwaongoza wachezaji kuvunja yai uwanjani hapo.

Vilevile KMC imetozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne badala ya watano kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mchezo kuelekea mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Kagera Sugar.

Related Posts