Nairobi. Kenya, imekuwa kimbilio kwa usalama wa wakimbizi na watu wanaohitaji hifadhi kutoka nchi zao, hasa wale wanaokimbia udhalimu wa kisiasa.
Hata hivyo, hali imeanza kubadilika kwa kasi na kuibua maswali mengi kuhusu usalama wa wageni nchini Kenya.
Katika miaka minne iliyopita, imekuwa ikishuhudiwa utekaji na mauaji ya raia wa kigeni nchini Kenya, jambo linaloathiri sifa ya Taifa hilo kama kimbilio salama kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi.
Takriban raia 50 wa kigeni wametekwa nyara au kuuawa katika ardhi ya Kenya, hali inayochochewa na mikataba ya siri ambayo imewaacha mikononi mwa maadui.
Miongoni mwa waathiriwa wa matukio hayo ni Maria Sarungi, mwanahabari na mwanaharakati kutoka Tanzania, aliyetekwa na watu wanne wenye silaha jijini Nairobi.
Maria akiwa na hali ya kuchanganyikiwa, aliachiwa baada ya kuzungushwa huku na kule na kuhojiwa kwa saa kadhaa. Hakuweza kutambua mahali alipokuwa ameachiwa, akieleza hakuwa na mwelekeo.
Tukio la kutekwa Maria lilitokea takribani miezi miwili tangu mwanasiasa wa Uganda, Kizza Besigye alipotekwa Nairobi na kusafirishwa kwa siri hadi mahakama ya kijeshi nchini mwake.
Besigye, mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alishtakiwa katika Mahakama ya Kijeshi kwa kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria, kosa linalodaiwa kutendwa Kenya.
Haijabainika kwa nini alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi ya Uganda kwa kosa linalodaiwa kufanyika Kenya.
Historia ya ulinzi wa wageni
Kenya ilikuwa na historia ya kutoa hifadhi kwa wale wanaokimbia mateso katika nchi zao.
Mfano, Rais Museveni na mkewe Janet walikimbia Uganda katika miaka ya 1970 wakihofia utawala wa kidikteta wa Idi Amin.
Walipofika Kenya, walikuwa salama na walikubalika kwa urahisi. Kenya ilikuwa sehemu salama kwa wageni, bila kujali tofauti za kisiasa na kijamii.
Hata hivyo, mabadiliko makubwa yamejitokeza katika kipindi cha miaka michache iliyopita. Raia wa kigeni kutoka nchi za Uturuki na Uganda wamekuwa waathirika wa matukio ya kutekwa.
Raia wa Uturuki, Mustafa Genç, Abdullah Genç, Hüseyin Yesilsu, Necdet Seyitoglu, Oztürk Uzun, Alparslan Tascı, na Saadet Tascı walitekwa nchini Kenya katika kipindi cha miezi mitatu tu iliyopita.
Raia hawa walikuwa wakimbizi chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa, lakini walikamatwa na kusafirishwa kurudi nchini mwao, ambako walishtakiwa na kufungwa jela.
Kama haitoshi, Selahaddin Gulen, mpwa wa Fethullah Gulen ambaye ni kiongozi wa harakati, alitekwa nchini Kenya na kusafirishwa hadi Uturuki. Fethullah Gulen alifariki dunia Oktoba 2024.
Matukio hayo yanaonyesha Kenya imekuwa sehemu ya shughuli za kisiasa za kimataifa, huku ikiwa na maelekezo ya kisiasa kutoka kwa mataifa kama Uturuki.
Uhusiano wa Kenya na Uturuki umeendelea kuimarika, moja ya mifano ni mkataba wa kijeshi uliotiwa saini kati ya mataifa hayo.
Mkataba huu unahusisha vifaa vya kijeshi na ushirikiano wa kiusalama.
Hata hivyo, mkataba huo umekuwa na athari kwa usalama wa raia wa kigeni, hususan wanaotoka katika nchi za Uturuki na Uganda. Hii inaonyesha kwamba, Kenya imekuwa ni sehemu ya vita vya kisiasa na kijeshi vinavyohusisha mataifa ya kigeni.
Katika tukio lingine, wanachama wa chama cha upinzani cha Uganda, Forum for Democratic Change (FDC), walikamatwa nchini Kenya baada ya kuingia nchini humo kwa ajili ya mafunzo.
Walikuwa wanahusishwa na mpango wa kumng’oa Rais Museveni madarakani. Walishutumiwa kwa kuhusika na ugaidi. Kesi dhidi yao bado inaendelea.
Matukio ya kutekwa nchini Kenya yameendelea kuongezeka, baadhi ya waathirika ni wanaharakati, waandishi wa habari na wanasiasa kutoka mataifa ya jirani.
Miongoni mwa hao ni Yusuf Ahmed Gasana, mwanaharakati wa Rwanda, ambaye alitekwa nyumbani kwake Nairobi na kisha kuhamishiwa Rwanda, ambako alikamatwa.
Pia, Morris Mabior Awikjok Bak kutoka Sudan Kusini alitekwa na maofisa wa Kenya na Sudan Kusini kabla ya kufukuzwa nchini kwake.
Mwanahabari maarufu wa Pakistan, Arshad Sharif, alikimbilia Kenya akitafuta hifadhi, lakini aliuawa kwa kupigwa risasi na maofisa wa polisi wa Kenya, jambo lililozua mashaka kuhusu usalama wa wageni nchini humo.
Taarifa za kukamatwa kwa Samson Teklemichael kutoka Ethiopia na Nnamdi Kanu kutoka Nigeria pia zimeongeza wasiwasi kuhusu hali ya usalama kwa wageni nchini Kenya.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matukio ya utekaji nyara nchini Kenya.
Hii ni changamoto kwa Kenya, hasa ikiwa inataka kudumisha hadhi yake kama kimbilio salama kwa wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi.
Roland Ebole, mtafiti wa Amnesty, alisema ongezeko la matukio hayo linatia doa sifa ya Kenya, hasa ikizingatiwa kuwa hivi karibuni ilichaguliwa kuwa sehemu ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.