Hatua kwa hatua uchaguzi wa Bavicha, Bazecha usiku kama mchana

Dar es Salaam. Makada wa Chadema, Deogratius Mahinyila na Suzan Lyimo wameshinda nafasi za uenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) na Wazee (Bazecha) katika uchaguzi uliokuwa na pilika pilika za hapa na pale.

Uchaguzi huo ulioanza asubuhi ya jana Jumatatu, Januari 13, 2025 umehitimishwa kwa nyakati tofauti leo Jumanne. Wa Bavicha uliokuwa na hekaheka nyingi umemalizika jioni huku wa Bazecha ulimazika asubuhi.

Uchaguzi wa Bavicha uliofanyikia ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam huku wa Bazecha ukifanyikia ukumbi wa makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini humo.

Msingi wa mchuano huo hususan wa Bavicha unatokana na makundi mawili ya wagombea uenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo dhidi ya Makamu mwenyekiti-bara, Tundu Lissu.

Mbowe na Lissu watachuana katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika Januari 21, 2025 huu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, kambi ya Lissu ndiyo imeibuka washindi kwa viongozi wapya wa Bavicha dhidi ya kambi ya Mbowe.

Mahinyila ameukwaa wadhifa huo kwa kupata kura 204, dhidi ya mshindani wake Masoud Mambo aliyepata kura 112, katika uchaguzi huo uliohusisha jumla ya wapigakura 317 halali na kura moja iliharibika.

Kwa upande wa Suzan, alipata kura 96, akiwashinda wenzake wanne akiwemo aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Hashim Issa aliyeambulia kura 14.

Wengine waliobwagwa na Lyimo ambaye katika uongozi uliopita alikuwa makamu mwenyekiti wa Bazecha bara ni John Mwambigija aliyepata kura 23, huku Hugo Kimaryo na Merchard Tiba wakipata kura tano kila mmoja.

Ushindi wa makada hao, umetoa turufu kwa kambi zote za uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Taifa, kati ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu, kwa kuwa Mahinyila ni mfuasi wa Lissu na Suzan wa Mbowe.

Hata hivyo, chaguzi hizo mbili zimeshindwa kutoa picha halisi ya nani kati ya Lissu au Mbowe aliye karibu na ushindi kuelekea uchaguzi wa Januari 21, mwaka huu, badala yake mizania imebaki sawa.

Ushindi wa Mahinyila inampa nafasi ya kumrithi, John Pambalu anayemaliza muda wake, huku Suzan akimrithi Hashim.

Ukumbini ushindi wa Mahinyila

Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Bavicha, Elisha Chonya alipomtangaza Mahinyila liliibuka shangwe na haikujulikana jina la ‘Lissu…! Lissu…! Lissu…!’ lililokuwa linaimbwa na wajumbe lilitokea wapi.

Zaidi ya nusu ya wajumbe walisimama kushangilia ushindi huo, huku wengine wakitupa vijembe kwa washindani wao kuwa, “tumeishinda rushwa.”

Uchaguzi huo, ulifanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Baada ya sauti ya mwenyekiti kusikika akisema shughuli ya kuhesabu kura imetamatika na ni wasaa wa kutoa matokeo wajumbe waliingia ndani na kutangaziwa kupewa zawadi.

Zawadi hiyo ni kofia ikiwa ni shukrani ya uvumilivu wao tangu shughuli waliyoianza jana asubuhi hadi asubuhi ya leo Januari 14 walipotangaziwa safu mpya ya uongozi waliyoichagua.

Ilikuwa ni nafasi yao ya kipekee kwa wajumbe hao kukutana kwa awamu ya pili huku wakinong’onezana na wengine wakishikana mikono kupiga picha za pamoja kama ishara ya furaha kwa kazi waliyoifanya.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu Mkuu Bazecha, imetangazwa kushikiliwa na Hellen Kayanza kwa kura 115 ambaye awali alikuwa akitumikia wadhifa wa naibu katibu mkuu bara.

Hellen amewabwaga washindani wake watatu, walioingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo akiwamo Casmir Mabina 10 na Leonard Mao kura 13.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti bara aliyeshinda ni Shaban Madede kwa kupata kura 123 ambaye aligombea peke yake na utaratibu alipigiwa kura ya hapana na ndiyo.

Vile vile kwa nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar, Hamoud Mohammed ametangazwa mshindi kwa kura 105 akimbwaga mpinzani wake Mohammed Haji aliyepata kura 33.

Katika nafasi ya naibu katibu mkuu bara, mshindi ni Hamida Mfaligunda akipata kura 103 akimbwaga mshindani wake wa Omary Mkama aliyepata kura 30.

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Rajab Bakari ameshinda kwa kura 117. Kwa jumla uchaguzi wa Bazecha haukuwa na pilika pilika nyingi kama wa Bavicha.

Kwa upande wa Bavicha, uchaguzi huo ulihusisha nafasi za Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar.

Katika uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa Bavicha Bara, Necto Kitiga ameongoza kwa kura, akiwapiku wenzake wanne.

Necto ameongoza kwa kupata kura 101, akichuana karibu na Juma Ng’itu aliyepata kura 90.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo ni Mkola Masoud aliyepata kura 32 sawa na asilimia 10, Nice Sumari aliyepata kura 47 sawa na asilimia 14 na Vitus Nkuna akipata kura 24 sawa na asilimia 7.5.

Hata hivyo, kuongoza huko hakukumwezesha Necto kushinda nafasi hiyo kwa kuwa hakufikisha zaidi ya asilimia 50 ya kura, hivyo uchaguzi uliotangazwa kurudiwa.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti Zanzibar, nafasi iliyokuwa na mgombea mmoja, Abdallah Haji ameshinda kwa asilimia 90 ya kura za ndio.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Suzan amewashukuru wajumbe waliothubutu kugombea nafasi mbalimbali huku akiwataka kila mmoja kutambua wajibu wake.

“Kamwe tusiwe chanzo cha chokochoko bali tusimame katika kama wapatanishi,” amesema.

Amesema baada ya kuona vipaji vya wagombea mbalimbali wakati wanajinadi ameahidi baada ya kuanza kazi atatoa fursa kwa wenye ujuzi kuwasilisha wasifu wao ili wachaguliwe kulitumikia baraza hilo.

Kwa upande wa Mahinyila amewashukuru wote walioshiriki mchakato huo kuanzia mwanzo hadi jana walivyohitimisha, huku akimshukuru mpinzani wake wa karibu Masoud Mambo.

“Nawashukuru sana tulikuwa na uchaguzi wa kidemokrasia, lakini ulikuwa na changamoto mbalimbali tulizojitahidi kukabiliana nazo.Tunaamini haki imeshinda na vijana wameshinda na wameonyesha namna ya kukilinda Chadema,” amesema Mahinyila.

Mahinyila amesema atakwenda kuilinda Chadema na kupigania haki, kwa sababu chama hicho kimebeba matumaini ya Watanzania.

Mambo adai rushwa ilitawala

Akizungumza na Mwananchi baada ya matokeo, Mambo amesema mchakato umekwisha na anajipanga kuzungumza na umma kueleza kwa kina kilichojiri akisema kulikuwa na viashiria vya rushwa.

“Uchaguzi umekwisha waliokuwa washindi ni washindi ila nina mengi ya kuongea kwa sababu mchakato huu uliingiliwa na watu wazito wale wanaojiita wapenda haki na wakemea rushwa lakini wao ndio wamekuwa wakitoa rushwa.

“Nitaeleza kwa kina namna mazingira yalivyokuwa ya rushwa katika uchaguzi huu, hiki kinachofanyika hapa sio cha kidemokrasia, hawa wanaolaumu hakuna haki ndiyo wala rushwa wakubwa,” amedai Mambo.

Suzan, Mahinyila ni kina nani?

Suzan kabla ya nafasi hiyo, alikuwa makamu mwenyekiti wa Bazecha bara na spika wa bunge la wananchi la Chadema.

Amewahi pia, kuwa mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya Chadema.

Kwa upande wa Mahinyila, kitaaluma ni wakili na amekuwa akihudumu katika kitengo cha sheria cha chama hicho kwa kujitolea.

Mahinyila amewahi kugombea udiwani wa Mpwapwa mkoani Dodoma mwaka 2020 na kukaa jela kwa miezi kadhaa kabla ya kuachiwa.

Akizungumza kabla ya matokeo, Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, Salum Mwalimu amesema wamesimama ndani ya kanuni na ndiyo sababu ya hatua njema iliyofikiwa.

Katika usimamizi huo wa kanuni, amesema wapo waliokwazika lakini hadi uchaguzi unaisha kila mmoja yuko salama.

“Tutaendelea kuomba utulivu wenu ili tuukamilishe uchaguzi wetu kwa asilimia 100,” amesema.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi, Dk Azavaeli Lwaitama ameanza hotuba yake kwa kuwaomba radhi wote waliokwazika kwa msimamo wake wa kufuata kanuni na katiba ya chama hicho.

Amesema uthubutu na ujeuri wa ujana ni jambo jemba, ingawa unapohitajika kuwa na nidhamu hakikisha unakuwa nayo.

“Wale waliokuwa wanaeneza mambo ya ajabu juu ya watu kama sisi na uadilifu wetu, watashangaa matokeo yatakapotangazwa,” amesema Dk Lwaitama.

Sintofahamu lango la ukumbi

Saa chache kabla ya kutangaza matokeo, sintofahamu imeibuka kwa wafuasi kusukumana na walinzi mlangoni, wakishinikiza wajumbe halali wa mkutano huo waliokuwa mlangoni waruhusiwe kuingia.

Sambamba na hilo, wafuasi hao mlangoni walifurika wakisukumana na kuzozana na walinzi, kushinikiza matokeo yatangazwe kwani kura zilishahesabiwa.

Mzozo mlangoni hapo, uliochukua takriban dakika 20 na baadaye palitulia baada ya wajumbe halali kuruhusiwa kuingia ndani.

Dakika chache baadaye, walinzi na baadhi ya viongozi wa baraza hilo, walionekana wakitoka ndani ya ukumbi na masanduku yaliyokuwa na kura ndani yake.

Hilo liliibua shaka kutoka kwa wafuasi waliokuwa nje ya ukumbi, hivyo walizuia masanduku hayo yasipakiwe kwenye magari kupelekwa popote.

Tukio hilo pia, liliibua mzozo mwingine, hadi hapo uongozi wa uchaguzi huo ulipoamua kuyarudisha ukumbini masanduku hayo.

Baada ya mvutano na mizozo katika lango la kuingia ukumbi wa mkutano, hatimaye wanahabari waliruhusiwa kuingia kusikiliza matangazo ya matokeo.

Kelele kutoka kwa mjumbe mmoja hadi mwingine zilisikika, wengine wakishangilia ushindi bila kujulikana unamuhusu mgombea yupi hasa.

Kwa jumla hali ya ukumbini haikuwa imetulia kutokana na idadi kubwa ya wajumbe waliokuwa wamesimama kusubiri matokeo hayo.

Usiku wa uchaguzi wa Bavicha, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam ilikuwa mithiri ya mchana wa Soko la Kariakoo.

Hiyo inatokana na mishemishe na pilika zilizoshuhudiwa zikifanywa na kila aliyekuwepo nje ya ukumbi, mara huku mara kule.

Kwa waliokuwa nje, isingekuwa rahisi kuwatofautisha na maofisa wa huduma kwa wateja, muda wote walionekana kuongea na simu.

Wengine walikaa vikundi vikundi na mmoja mmoja alihama kutoka kikundi kimoja hadi kingine baada ya dakika chache.

Ukiachana na waliokuwa nje, safari za kuingia na kutoka ukumbini zilitawala kwa wajumbe wa mkutano huo, baadhi wakienda chooni na wengine wakielekea uelekeo wa Shekilango.

Safari hizo za chooni na kuelekea Shekilango, hazikuwa za mjumbe mmoja mmoja, walikwenda kwa makundi ya watu kati ya watano hadi sita.

Ingia toka hizo, zilinoga zaidi ilipofika saa sita usiku baada ya kukamilika kwa uhakiki wa wajumbe wa mkutano huo na haikujulikana wanafuata nini.

Walipoulizwa baadhi ya wajumbe kuhusu wanachokifuata uelekeo wa Shekilango walijibu wanakwenda kununua chakula na baadhi yao walionekana wakirudi na maji mkononi.

Haikuishia hapo, muda mchache baadaye gari zilizobeba makada na baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema, zilianza kuingia na kila moja iliegeshwa maeneo ya Ubungo Plaza.

Viongozi na makada hao waandamizi ni miongoni mwa wanaowaunga mkono wagombea wa uenyekiti, Masoud Mambo na Deogratius Mahinyila.

Kuwasili kwa gari hizo, kuliongeza kasi ya ingia toka za wajumbe ukumbini, hadi Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Salum Mwalimu alipowahoji kunani nje na kuamrisha milango ifungwe na atakayetoka asiruhusiwe kuingia.

Hata hivyo, onyo hilo halikutosha kuwazuia wajumbe kutoka na kuingia ukumbini humo na safari zao zilikuwa na uelekeo ule ule.

Baadhi ya wajumbe walizungumza na gazeti hili, walilalamikia kupokea jumbe nyingi za mambo ya kura kutoka kwa kambi za wagombea mbalimbali.

Ulikuwa usiku ambao aghalabu watu huutumia kulala, lakini hali ilivyokuwa nje ya Ubungo Plaza kila mmoja alichangamka kwa namna yake.

Ukiachana na pilika hizo, kulitokea mshikemshike uliofanya karibu vijana watushiane ngumi, baada ya madai ya mmoja wa wagombea, Idrisa Rubibi kutoa nauli kwa wajumbe.

Hilo lilisababisha baadhi ya wajumbe wahoji, kwanini mgombea huyo anatoa nauli hizo, lakini baadaye Bavicha ilifafanua hizo zilikuwa posho ambazo wajumbe hao walikuwa hawakulipwa.

Hata hivyo, Rubibi kupitia mtandao wake wa kijamii, amesema kinachoelezwa ni upotoshaji kwani alipewa jukumu la kuwahudumia viongozi waliotoka kwenye kanda ya magharibi kwa kuwapa mahitaji yao ambayo ni stahiki zao nauli na malazi.

“Kuhusu kwamba mimi ni mgombea sipaswi kupewa majukumu/katiba yetu haijakataza kiongozi kuto timiza majukumu yake hata kama anagombea,” amesema.

Mvutano mwingine ulionekana saa 12 asubuhi, baada ya kambi za wagombea hao, kati ya Mahinyila na Mambo wakituhumiana kutoa rushwa kwa wajumbe.

Hali ya kurushiana maneno ilishuhudiwa katika eneo hilo, kati ya kambi hizo mbili nje ya ukumbi wa mkutano huo.

Vituko, mbwembwe za wagombea 

Mbwembwe zilikuwa sehemu ya sera za wagombea wa nafasi hizo na kuibua vicheko kutoka kwa wajumbe waliokuwepo ndani ya Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Vituko vilianza kushuhudiwa kutoka kwa mgombea wa ujumbe wa mkutano mkuu Bavicha Zanzibar, Alawiya Shaibu Hussein ambaye hakuwa na muda wa kumwaga sera, baada ya kujitambulisha aliishia kusema anaomba kura.

Kimbembe kilikuwa wakati wa kujibu maswali, aliulizwa iwapo atakusanya yote ndipo ajibu alimwambia msimamizi wa uchaguzi, “wewe endelea,” bila kujibu swali.

Kama ilivyokuwa kwa swali la kwanza, mgombea huyo alishindwa kujibu, licha ya kuomba lirudiwe.

Aliulizwa swali la tatu kwamba atakifanyia nini chama hicho iwapo atachaguliwa amejibu, “kuhamasisha na kuhamasisha vijana.”  

Ulipofika wakati wa mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Najma Hemed Ali ameanza kwa kujitambulisha jina na nafasi aliyonayo sasa, kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa, hivyo kusababisha minong’ono kutoka kwa wajumbe.

Msimamizi wa uchaguzi alipowataka wajumbe wawe watulivu, mgombea huyo alianza upya kujieleza kwa kusema, ” vijana naomba kura zenu.”

Ameendelea kwa kuwahoji wajumbe, “mmekubali au, kweli? Aya Asante.”

Hayo yalisababisha vicheko kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi.

Alipoulizwa swali la kwanza, Najma alikaa kimya, vivyo hivyo kwa swali la pili na tatu.

Mbwembwe hizo hazikuishia kwenye kushindwa kuzungumza, bali hata aina ya maneno na mtindo wa uombaji kura.

Miongoni mwa wagombea waliotia mbwembwe katika kumwaga sera zake ni Pascal Mlapa anayeutaka ujumbe baraza kuu Bavicha, bara.

Ameanza sera zake kwa kuitambulisha taaluma yake ya ujenzi wa maghorofa, akiihusisha na kile alichosema kama anajenga maghorofa atashindwa kujenga hoja.

“Kama najenga maghorofa nitashindwa kujenga hoja ndugu wajumbe?” amesema Mlapa.

Sambamba na hilo, ameahidi kuhakikisha anaitibu kile alichokiita malaria iliyopo ndani ya chama hicho, kwa kusimamisha nguvu ya umma.

Atasimamisha nguvu ya umama kuchochea mabadiliko aliyodai yatatibu malaria iliyopo ndani ya chama hicho.

Amesema haiwezekani afike katika baraza kuu la chama hicho kikuu cha upinzni kisha aseme sawa bwana mkubwa, wakati akidai vijana wanatekwa na hatakubali kubaariki biashara hiyo.

Kwa upande wa Barnaba Samwel anayegombea nafasi hiyo, amejinadi kwa kutaja nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika ikiwemo Mwenyekiti wa Chadema Tawi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam.

Amesema amewahi pia kuwa mhazini wa mtandao wa wanafunzi Mkoa wa Dar es Salaam, amewahi kugombea uenyekiti kanda ya Dar es Salaam na kwamba anaomba ridhaa.

Wingi wa nyadhifa alizowahi kushika, umesababisha swali kutoka kwa mmoja wa wajumbe aliyemuuliza amewahi kufanya nini katika nafasi hizo, amejibu, “kwa sasa yeye ni mkunja ngumi kama wakunja ngumi wengine.”

Hata hivyo, mgombea huyo hakumaliza sera zake, alikatishwa na msimamizi wa uchaguzi kutokana na muda wake wa dakika mbili alizopewa kumalizika.

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo ni Ezekiel Mollel aliyesema amewahi kuwa spika wa bunge la wanafunzi IFM na sasa ni Katibu wa Baraza la Vijana Kigamboni.

Amesema ameomba nafasi hiyo kwa sababu ya matamanio ya kuwepo baraza litakaloaminika tena na kuwavutia vijana.

Kwa upande wa Atfat Hamad Ali anayeutaka ujumbe huo kutokea Zanzibar uombaji kura wake ulihusisha mikono na mbwembwe za kuvuta sauti.

Sambamba na hilo, mgombea huyo hakutumia hata dakika moja kati ya mbili alizopaswa kumwaga sera zake.

Kabla ya msimamizi wa uchaguzi hajaamrisha maswali kuulizwa, Atfat tayari alishaomba wajumbe wamuulize.

Hilo liliibua vicheko kutoka kwa wajumbe, ambao wamezoea utaratibu wa maswali hutangazwa na msimamizi wa uchaguzi.

Katika moja ya maswali aliyoulizwa, mgombea huyo alimwamrisha mjumbe anayeulizwa swali asimame ili amwone ndiyo amjibu.

Katika kuzimwaga sera zake, Halfan Abdallah Maalim anayeutaka ujumbe wa mkutano mkuu Bavicha Taifa, ameshindwa kuitaja nafasi anayoiomba, huku akishindwa kuongea kwa ufasaha mbele ya kadamnasi

“Nimesimama hapa kugombea nafasi ya mjumbe mkuu… Mjumbe wa mkutano Mkuu Bavicha Taifa, naombeni kura zenu,” amesema.

Hata hivyo, ameshindwa kuendelea na sera, badala yake aliamua kuomba kura moja kwa moja.

Wakati wa maswali, mgombea huyo alitaka yaulizwe yote kisha ayajibu kwa pamoja na aliishia kujibu swali moja lililohusu uzoefu wake ndani ya chama hicho.

Imeandikwa Baraka Loshilaa, Tuzo Mapunda, Bakari Kiango na Juma Issihaka

Related Posts