Unguja. Madereva wa magari ya utalii Kijiji cha Kendwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja wameiomba Serikali kuwapatia eneo la maegesho ya magari ili kuondokana na usumbufu unajitokeza.
Wamezungumza hayo katika kikao cha Katibu Tawala Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, leo Januari 14, 2025, kilichowakutanisha madereva hao kuzungumzia changamoto mbalimbali.
Dereva Abdulla Abdi Ahmada amesema awali walikuwa na utaratibu mzuri wa kuegesha magari yao kwa sababu kulikuwa na kiwanja maalumu na magari hayo yalikuwa katika usimamizi wa wanakijiji hicho.
“Awali, wanakijiji walikuwa wameweka utaratibu wa kuzisimamia na kuziweka katika kiwanja kilichokuwepo maeneo ya fukwe (Mivinjeni) na magari haya yalikuwa yanatozwa fedha na kuingia kijijini ila kwa sasa hatuna eneo maalumu la kuegesha magari ndio sababu ya gari hizi kupakiwa bila ya utaratibu,” amesema Abdulla.
Dereva mwingine, Abdullareem Salum Kombo amesikitishwa kuondolewa huduma za maegesho ya magari katika eneo hilo, jambo ambalo limerudisha msongamano na uwekaji holela wa magari hayo.
Naye, Sheha wa Kilindi, Ibrahim Maabad Juma amekiri kuwepo kwa tatizo la uwekaji mbaya wa magari yanayopeleka wageni kwa ajili ya utalii hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Katibu Tawala Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Maryam Said Khamis ametoa agizo kwa uongozi wa baraza la manispaa ya wilaya hiyo kuwatafutia maegesho maalumu madereva wanaopeleka watalii ili kuondoa msongamano wa magari.
Amewataka madereva kuacha kuegesha magari pembezoni mwa barabara ili kuepueka msongamano na ajali.
Maryam amesema Serikali imeamua kuzijenga barabara za ndani hasa sehemu za uwekezaji ili kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.