Njombe. Kamati ya Shule ya Msingi NjooMlole iliyopo Halmashauri ya Mji wa Njombe imewataka wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa kuhakikisha wanawanunulia watoto wao vifaa vinavyohitajika shuleni ikiwamo sare za shule, madaftari na kupeleka vyakula shuleni ili wasome kwa uhuru na kufaulu masomo yao.
Hayo yamesemwa leo Januari 14, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi NjooMlole Raymond Mwageni wakati akipokea vifaa vya shule ikiwamo madaftari, kalamu na majaba ya kuweka maji kutoka kwa Diwani wa Uwemba, Jactan Mtewele ili kuleta motisha kwa wanafunzi kuweza kufanya vizuri na kufaulu masomo yao.
Amesema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha mahitaji ya watoto wao shuleni yanapatikana ili waweze kusoma vizuri bila ya kuwa na mawazo mengine tofauti na shule.
Amesema mwanafunzi anapokosa mahitaji muhimu ya shule wakati wenzake wanayo kiuhalisia huwa anakosa raha na kuwa mnyonge, hivyo kumsababishia msongo wa mawazo na hata kushindwa kusoma na kufanya vizuri.
“Naiomba Serikali iweze kutusaidia wale wazazi ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wa kuchangia chakula ambacho wanatakiwa wapate watoto shuleni, niliomba nguvu itumike ikiwamo kutolewa adhabu ili waweze kutoa mahitaji kwa wakati,” amesema Mwageni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi NjooMlole Atuswege Mwambela amesema wameendelea kuhamasisha wazazi kila siku kuwapa watoto wao mahitaji muhimu ya shule.
Amesema wazazi wanaposhindwa kuwapa mahitaji watoto wao inawavunja moyo kwa kiasi kikubwa kwa kuwa, suala la elimu ni tofauti na vitu vingine kwani unapomfundisha mtoto lazima upate mrejesho kupitia mitihani sasa kama hana madaftari au peni ni wazi kuwa hawezi kufanya vizuri.
“Viongozi wanapofanya hivi wanatutia moyo sisi watenda kazi kwani tunajisikia vizuri na tunapata ari ya kufanya kazi” amesema Mwambela.
Diwani wa Uwemba, Jactan Mtewele amesema ametoa msaada Shule ya Msingi NjooMlole kwa sababu ni moja kati ya shule zinazofanya vizuri kwenye masomo katika kata hiyo na kuiletea heshima.
Amesema ametoa msaada huo kama motisha kwa wazazi ambao mpaka shule inafunguliwa mzazi anashindwa kumnunulia mahitaji ya muhimu mtoto wake ikiwamo sare za shule , madaftari pamoja na peni kwa ajili ya kuandikia.
“Nimefanya hivi kuwapa taarifa wazazi kuwa huu ni wajibu wao wakishirikiana na sisi viongozi, tunapaswa kuwajibika kutoa mahitaji muhimu yote kwa wanafunzi wetu,” amesema Mtewele.
Constatino Ndonyaro ambaye ni mwanafunzi wa shule hiyo amesema vifaa walivyopatiwa na diwani huyo vitawasaidia kusoma vizuri na kufaulu mitihani yao, hivyo kuwaomba wazazi kujitahidi kuwasaidia watoto wao kupata vifaa vya darasani.
“Wazazi wajitahidi kuwapatia watoto vifaa vya darasani kama daftari, peni rule na mikoba,” amesema Ndonyaro.