Miradi ya ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha  mabasi yaanza Mbeya

Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya limeanza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikijumuisha ujenzi wa soko la kisasa la Matola, kituo kipya cha mabasi ya mikoani na eneo la uwanja wa ndege wa zamani ulipo Kata ya Pambogo.

Miradi hiyo inayogharimu  Sh31 bilioni, inafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), huku Jiji la Mbeya likiwa ni mojawapo ya maeneo sita nchini yanayonufaika na ufadhili huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema hayo leo Jumanne Januari 14, 2025 kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ambaye amekagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.

Nchimbi amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa kasi nzuri na inatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2025.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amepongeza miradi hiyo ya kimkakati huku akiishukuru Serikali na mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson.

Issa amesema miradi hiyo itaboresha maisha ya wananchi kwa kutoa huduma za kisasa kupitia soko na kituo cha mabasi kilichoboreshwa.

Kwa upande wake, Homera amemsisitiza  mkandarasi kutobweteka kwa sifa bali apambane kuhakikisha anakamilisha miradi hiyo ikiwa na ubora na kwa wakati.

“Nimesikia kuna wizi wa vifaa vya ujenzi, sasa nawaonya wote wanaojihusisha na wizi huo, tukiwakamata hakutakuwa na huruma bali hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesema Homera.

Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara wa mbogamboga aliyekutwa eneo la mradi, Sekele Laudence ameiomba Halmashauri ya Jiji kuhakikisha  wazawa wanapewa kipaumbele baada ya kukamilika kwa miradi hiyo ili kuzuia migogoro.

Miradi hiyo inalenga kuboresha huduma kwa wananchi na kukuza uchumi wa Jiji la Mbeya.

Related Posts