Dar es Salaam. Kampuni 20 za uwekezaji kutoka nchini Japan zimekuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji katika maeneo ya kilimo, utalii na sekta ya uzalishaji viwandani ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kampuni hizo zimekutana na nyingine 50 za Kitanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu, teknolojia sambamba na kufanya biashara kwa pamoja kwa kuingia miradi ya ubia.
Wawekezaji hao wapo nchini huku thamani ya uwekezaji wa kampuni za Kijapan kwa miaka 12 iliyopita umefikia Dola 11.4 milioni za Marekani (Sh28.8 bilioni) kwenye miradi 24 iliyosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji (TIC), huku zikizalisha ajira zaidi ya 1000.
Akizungumza wakati akifungua kongamano hilo la uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Japan lililofanyika leo Jumanne Januari 14, 2025 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema hatua hiyo ni muhimu kwa Tanzania kwenye sekta ya uwekezaji.
“Tanzania na Japan, tuna uhusiano wa muda mrefu katika biashara na zaidi kwenye miradi ya maendeleo kwenye sekta ya viwanda na barabara,” amebanisha.
Amesema Japan imeendelea kuwa wabia wakubwa wa maendeleo kwa kuwa, wanaingiza bidhaa zao ikiwamo magari na bidhaa za kieletroniki huku Tanzania pia ikisafirisha malighafi na bidhaa za kilimo zikiwamo zilizochakatwa kama chai na kahawa.
“Tunaingiza sana magari kutoka Japan sasa tungependa baadhi ya magari na vipuri vizalishwe hapa hapa Tanzania. Pia, tuwe tunapeleka kwao bidhaa na si malighafi inabidi zichakatwe hapahapa” amesema Kigahe.
Amesema faida ya hilo ni kuongeza ajira nchini, teknolojia ya kisasa pamoja na kuuza nje bidhaa ambako italeta fedha za kigeni.
Amesema katika kuendeleza uhusiano huo kwa sasa wafanyabiashara wa Tanzania na Japan watakaa kwa pamoja kujifunza na kuwa na ushirikiano kwa kuwa Wajapan wana teknolojia za hali ya juu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Hisayuki Fujii amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uhusiano mzuri wa kibishara na kidiplomasia na nchi mwao.
“Uhusiano wa nchi hizi mbili umezidi kuwa karibu zaidi ni jambo la kujivunia nitumie fursa hii kwa Serikali za nchi zote mbili sambamba na mkutano huu wa wawekezaji unaofungua fursa mpya,” amesema.
Mwekezaji Yoshiyuki Mizouchi kutoka Kampuni ya Tanja iliyowekeza Karatu amesema amekuwa balozi wa kampuni za Kijapan ili kuzivutia zije kuwekeza kama wao.
“Kampuni yetu inajihusisha kwenye kilimo tupo tangu 2023 tumetoa ajira kwa Watanzania. Matamanio yetu Wajapan wengine waje kuwekeza zaidi,” amesema Mizouchi.
Naye, Hans Kejo kutoka Kampuni ya Hamidu City Park amesema watashirikiana na kuwatumia wageni hao hususani katika sekta ya teknolojia.