Hakuna hata mmoja aliyekamilika katika idara zote, isipokuwa Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana familia ina baba, mama na watoto. Timu ya mpira wa miguu inaundwa na watu tofauti, wakiwemo makipa, walinzi, viungo na washambuliaji. Serikali nayo inaundwa na wanasiasa, watendaji, wasimamizi na idara nyingine. Yote hayo ni kuhakikisha mawazo tofauti yanatumika kujenga.
Ipo hadithi ya mfalme aliyekosa subira kiasi cha kukorofishana na raia wake wote. Alikuwa akiona kila awazalo na atendalo ni jema, lakini akawaona wenzake wakitenda ndivyo sivyo. Washauri wake, akiwemo Waziri Mkuu walijaribu kila wawezavyo kumwonesha kuwa maisha hayapo kama tunavyoyaona binafsi, lakini wote waliishia vitanzini kwa kunyongwa. Wananchi walipolalamika wakanyongwa, wanyongaji walipouliza maswali nao wakanyongwa!
Hatimaye nchi ikabaki pweke. Mfalme akakosa mtu wa kumtawala, hivyo akaamka alfajiri kujaza makasiki ya maji ya kunywa na kuoga, akafagia kasri pamoja na viwanja vyake, akajipikia na kuosha vyombo mwenyewe na baada ya hapo aliketi barazani. Kwa kuwa hakukuwa na mtu wa kuleta malalamiko wala pongezi, aliondoka mapema kutembea mtaani pasipo na watu kisha akaja kulala. Maisha hayo yalimtia unyonge. Akaanza kumwomba Mwenyezi Mungu amshushie raia wapya na kuahidi kutowatenda vibaya.
Kwa bahati siku moja alipita walii mjini pale. Akashangaa kuona mashamba yamefunikwa na vichaka na milango imetandwa na buibui. Akajivuta panapo kasri la Mfalme na kumkuta amebarizi viungani. Kabla hajampa salamu ya heshima, Mfalme alianguka miguuni pa walii na kumsihi amwombee msamaha kwa Maulana kwa makosa yake. Alitubu madhambi na kuahidi kutokuyarudia.
Baada ya Walii kusikiliza kisa chote cha Mfalme, akatumia busara kuamua. Aliwajua wanasiasa walivyo wepesi wa kusahau na wagumu kujifunza. Hivyo alichukua Jeshi la jirani na kumpindua Mfalme. Alimtawala akimtumikisha kama njia ya kumfunza uungwana, matumizi mazuri ya utawala na kumcha Mungu. Bila shaka Mfalme aliona tofauti ya utamu wa kutumikiwa na uchungu wa kutumikishwa.
Wanasiasa ni watu wanaosahau mapema mara tu baada ya kuitwa waheshimiwa. Hapa Afrika alikuwapo rais mmoja wa aina hiyo katika nchi jirani na Tanzania. Wapinzani wake walimdai abadilishe katiba waliyoiona kuwa kandamizi kwa wananchi, yeye akagoma na kuitetea kuwa hiyo ni moja ya katiba bora zaidi duniani. Uchaguzi Mkuu ulipojiri akashindwa na mpinzani wake. Majuma machache tu yaliyofuata, Rais huyo aliyeshindwa katika uchaguzi aliilalamikia katiba ileile aliyoitetea mwanzoni.
Hivi karibuni tumeyaona na kuyasikia yaliyotokea Arusha. Mbunge aliyewahi kujizolea umaarufu mkubwa kwenye uongozi wa Tanzania aliyakanyaga mbele ya Mkuu wake wa Mkoa, ambaye pia ni maarufu kwenye hekaheka za siasa za kibongo. Ukweli ni kwamba Mheshimiwa Mbunge alitekeleza siasa za kibongo kama zilivyo, lakini bingwa akamchenjia gia hewani na kumtoa kwenye mstari.
Kiongozi alikuja mbele ya walalamikaji wakuu ambao ni wananchi, akaichomea Serikali yake kwa maswali mazito yaliyoitaka Serikali ijipambanue juu ya mradi wa barabara. Lakini kumbe alikuwa amesahau kuwa yeye pia ni mmoja wa viongozi wanaojifungia kutunga kauli za kutulainisha sisi wapigakura wao. Alipoulizwa iwapo alihudhuria vikao na kukumbushwa yale “mambo yao”, tuliona sura ikimpwaya.
Siasa haitofautiani na muziki kwenye mipango. Mwanamuziki yeyote ni lazima ajue namna anavyoingia kwenye jukwaa na namna atakavyoondoka hapo. Wenyewe wananielewa vizuri kwani anaweza kuipokea sauti ya juu sana, lakini akaichezesha kwa namna anavyokusudia kutoa ujumbe wake. Ipo namna ambayo wanasiasa hupokezana vijiti na kutuacha tusielewe kuwa wanaenda pamoja au wanatofautiana.
Ndege wa rangi moja huruka pamoja. Abadan wanamuziki wa bendi moja hawawezi kuimba tofauti. Lakini iwapo jukwaa moja litatumiwa na bendi kadhaa kwa wakati huohuo, ipo hatari ya bendi mahiri kuchanganywa kimawazo na mahasimu wao. Wazee wenzangu wanakumbuka sakata la bendi kuzimiana umeme katika miaka ya tisini pale bustani ya Mnazi Mmoja.
Siasa za kibongo zinatatanisha sana. Ipo siku wabongo tutadai midahalo ya ana kwa ana baina ya viongozi au wagombea mahasimu ili tupate ufafanuzi wa kutosha, badala ya kusikiliza malumbano yasiyo na mwisho kila mmoja akivutia upande wake. Hapa bongo tumewahi kushuhudia viongozi walio kwenye benchi la ufundi wakikimezea mate kiti cha urais. Na ndipo sasa tunashuhudia Mwenyekiti na Makamu wake wanachuana badala ya kupokezana kijiti!
Nijuavyo mimi, timu ya uongozi inakwenda na jambo moja. Mtafaruku wowote baina yao unaweza kuugawanya uongozi kama waendesha mashua wanaogombania mbao wakiwa katikati ya bahari. Abiria hawawezi kuwa salama. Na ili kujinusuru, mmegeko wa aina hiyo ni lazima uzimwe kikatiba kabla wanachama hawajaanza kuwa na wasiwasi iwapo wanaongozwa na watu makini au la.
Miiko ya uongozi ni lazima ifuatwe katika nyanja zote. Vyama na taasisi zote za uongozi ziwatathmini kwanza wateule wao kabla ya kuwaachia sukani kabla wasije kutupeleka mrama. Ndiyo maana wenzetu walioendelea hutazama sera za wagombea bila kuwa na wasiwasi na vyama watokavyo. Ni kwa sababu wana uhakika na weledi wa wagombea hao.