Sababu CAF kusogeza mbele Chan

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza kusogeza mbele fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan) 2024 zilizokuwa zifanyike Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28, 2025.

Taarifa iliyotolewa na CAF leo Jumanne, Januari 14, 2025 imeeleza kuwa kuahirishwa kwa Chan ni kutoa muda wa kukamilisha miundombinu kwa nchi waandaaji.

“Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) leo limetangaza kuahirishwa kwa Mashindano ya Mataifa ya Afrika ya TotalEnergies CAF (CHAN) Kenya, Tanzania, Uganda 2024 hadi Agosti 2025.

“Maendeleo mazuri yameonekana nchini Kenya, Tanzania na Uganda katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja, uwanja wa mafunzo, hoteli, hospitali na miundombinu mingine na vifaa kwa ajili ya mwenyeji wa mafanikio wa TotalEnergies African Nations Championship (CHAN) Kenya, Tanzania, Uganda 2024.

“Hata hivyo, wataalam wa wa ufundi na miundombinu wa CAF ambao baadhi yao wamekuwepo Kenya, Tanzania na Uganda, wameishauri CAF kwamba muda zaidi unahitajika kuhakikisha kuwa miundombinu na vifaa viko katika viwango vinavyohitajika kuandaa kwa mafanikio ya mashindano hayo kwa Kenya, Tanzania, Uganda 2024,” imefafanua taarifa hiyo ya CAF.

Rais wa shirikisho hilo, Patrice Motsepe amewashukuru Marais wa Tanzania, Kenya na Uganda kwa juhudi zao na sapoti kwa maandalizi ya mashindano hayo.

“Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa Rais William Ruto wa Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Yoweri Museven wa Uganda kwa uongozi wao, kujitolea na maendeleo mazuri ambayo yamefanywa katika ujenzi na kuboresha viwanja, uwanja wa mafunzo, hoteli, hospitali na miundombinu mingine na vifaa.

“Nimeshangazwa na ujenzi unaoendelea na ukarabati wa miundombinu ya soka na vifaa nchini Kenya, Tanzania na Uganda,” amesema Motsepe.

Motsepe alisema kuwa anaamini ifikapo Agosti, miundombinu itakuwa imekamilika tayari kwa kuziwezesha nchi hizo kuandaa Chan.

Awali mapema leo asubuhi, Januari 14, 2025  Mwenyekiti wa Kamati ya ndani ya maandalizi ya Chan upande wa Tanzania, Leodgar Tenga amesema Tanzania ipo tayari kuandaa mashindano hayo.

“Ili kufanikisha mashindano hayo, Serikali imefanya maandalizi muhimu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano hayo ambao umefanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa na Uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar.

“Vilevile kwa matakwa ya CAF vimejengwa viwanja vya mazoezi vya Gymkhana, Law School na Meja Jenerali Isamuhyo ambavyo vitatumika kwenye mashindano ya CHAN.

“Maandalizi haya ya miundombinu hii ya yamefikia asilimia zaidi ya tisini na tano.

“Ili kujiridhisha na maandalizi yanayofanyika Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (Caf) limekuwa likifanya ukaguzi wa mara kwa mara na wameridhishwa na maandalizi pamoja na utayari wa nchi yetu kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ingawa kuna mambo kadhaa tunaendelea kuyakamilisha,” amesema Tenga.

Fainali za Chan hufanyika kila baada ya miaka miwili na awamu hii inashirikisha nchi 19

Related Posts