KONA MALOTO: Ukimsikiliza Lissu kwa makini utamwomba msamaha Magufuli

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, anakabia juu katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa chama chake. Anahakikisha Mwenyekiti aliye ofisini kwa sasa, Freeman Mbowe, hapati nafasi na yeye ya kuanzisha mashambulizi.

Kilele cha uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chadema ni Januari 21, 2025. Mbowe anapambana kujibu hoja katika mfululizo wa mahojiano na vyombo vya habari. Lissu anatimua vumbi na kuchafua hali ya hewa kila Mbowe anapojitahidi kusafisha upande wake.

Januari 6, 2024, Lissu alirejea Tanzania, baada ya kuwepo Brussels, Ubelgiji, katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka 2024 na mwanzo wa 2025. Akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Lissu alizungumza mengi kuhusu tofauti zake na Mbowe.

Alisema, aliamua kugombea uenyekiti baada ya kugundua Mbowe amemwekea mpinzani kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti. Lissu alimtaja mpinzani huyo kuwa ni Ezekia Wenje. Lissu alisema: “Mimi nigombee na Wenje, nashindana na aliyemtuma. Sasa nagombea ya kwake.”

Kabla, Lissu alisema kuwa sababu ya kugombea uenyekiti Chadema ni mwenendo wa chama hicho. Kwamba kimeporomoka kisiasa, hivyo anataka kukiokoa. Alishasema kwamba Chadema anguko lake limesababishwa na maridhiano, ambayo chama hicho kilifanya na CCM, vilevile Serikali mwaka 2022 na 2023.

Kuna lawama nyingine kuwa uongozi mbaya wa Mbowe ndio umeiangusha Chadema. Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020 na Serikali za Mitaa 2024, maumivu yote ya Chadema, lawama ni kwa Mbowe.

Hiki ni kipindi ambacho CCM wanakenua. Wana utulivu mkubwa, wanapoelekea Uchaguzi Mkuu wao ndani ya chama, Januari 18 na 19, 2024. Jirani na mpinzani wao kunafuka moshi, wao ni utulivu mkubwa.

Hakuna raha kama kuona kwa adui kunawaka moto ndani kwa ndani. Inakufanya upumue, maana huna mpinzani. Pili, ni fursa ya kujipanga vizuri, ili adui atakapotaka kurudi kwenye mapambano, uwe unaufahamu udhaifu wake, umpige panapofaa.

Lawama za anguko la Chadema, zinazotolewa na Lissu, zinafanya CCM wajipange kukisambaratisha endapo Mbowe atashinda uenyekiti. Lawama zinazotolewa na timu ya Mbowe, zitawakong’ota pale Lissu atakapofanikiwa kukalia kiti. Ni somo kutoka kitabu cha “Thirty-Six Stratagems”, kilichoandikwa na Jenerali Wang Jingze, wa dola ya Southern Qi, China, Karne ya Tano. Sura ya kwanza ya kitabu yenye kichwa “Winning Stratagems” – “Ushindi wa Mbinu Chafu”, Jenerali Wang anafundisha kuhusu subira kipindi adui akiwa imara.

Subira hiyo, inasaidia kumfuatilia adui kujua wakati akikabiliwa na majanga au akiwa amezubaa, ili iwe rahisi kumshambulia na kumshinda. Ndivyo ilivyo sasa kwa CCM dhidi ya Chadema. Wanausoma mchezo ndani ya ngome ya mpinzani wao. Muda wa mapambano ukifika, haitakuwa salama kwa Chadema.

Yote mabaya yanayosemwa kuhusu Mbowe kutoka kwa Lissu, yatakuwa mtaji wa CCM, vivyo hivyo kwa Lissu, yanayoelekezwa kwake kutoka timu Mbowe. Tofauti ni moja, Lissu anamshambulia Mbowe moja kwa moja, wakati mashambulizi dhidi ya Lissu, yanatolewa na timu inayomuunga mkono Mbowe.

Mashambulizi mengine, hasa kutoka kwa Lissu, yanaisafisha CCM. Mathalan, hoja kubwa ya anguko la Chadema katika uchaguzi kuanzia Serikali za Mitaa 2019 ni kile ambacho wamekuwa wakikiita “uchafuzi” badala ya uchaguzi. Kwamba vyama vya upinzani viliporwa.

CCM wapo kwenye nafasi nzuri ya kutamba kuwa kila uchaguzi ambao Chadema wanaulalamikia, walishinda kihalali, kwani hata wao Chadema ndani kwa ndani, wanamshutumu Mbowe kwa kuwaongoza vibaya, chama kikapoteza mvuto, wakashindwa uchaguzi.

Ni kipindi ambacho, ukimsikiliza Lissu dhidi ya Mbowe, utatamani kumwomba msamaha Rais wa Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli. Kumbe alisingiziwa kudhulumu uchaguzi Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020. Utamwondoa kwenye lawama Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kilichotokea Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024.

Tatizo halikuwa Magufuli wala Rais Samia, bali Mbowe. Hivyo ndivyo namwelewa Lissu. Ukifika hapo, unaweza pia kujenga muktadha kwamba hata wabunge 19 wa Chadema, walioapishwa kuwa wabunge, nao walionewa.

Wabunge hao, waliripoti bungeni na kuapishwa, wakati msimamo wa Chadema ulikuwa kuyapinga matokeo. Kipindi hiki ambacho Mbowe anatajwa kuwa uongozi wake umedidimiza chama, yupo mtu anawaza kumbe matokeo 2020 yalikuwa ya haki, Chadema walipata walichostahili. Kwa maana hiyo, Halima na wenzake hawakukosea kwenda bingeni.

Coattail Effect ni nadharia ya uchaguzi, ambayo maana yake ni matokeo ya mgombea katika nafasi ya juu, kuwa na ushawishi mkubwa kwa wagombea wa nafasi za chini.

Mathalan, mgombea Urais anakuwa na nguvu kubwa, hivyo kishindo chake kinawabeba wagombea ubunge wa chama chake mpaka madiwani. Coattail Effect inaweza pia kubeba tafsiri ya mgombea ubunge kuwabeba wagombea udiwani katika kata za jimbo lake la uchaguzi.

Coattail Effect kwa maneno mengine huitwa Down-Ballot Effect, kinyume chake ni Negative Coattail Effect, kwamba ushawishi mdogo wa mgombea wa juu, unawaathiri wagombea wa chini, hivyo kupoteza viti vingi.

Nadharia ya Coattail Effect inakamilishwa na Reverse Coattail Effect, ambayo maana yake ni wagombea wa chini kumbeba wa juu. Kwamba mgombea Urais anabebwa na wagombea ubunge, vivyo hivyo kwa mgombea ubunge dhidi ya wagombea udiwani jimboni kwake.

Kama hoja ni Uchaguzi Mkuu 2020, Magufuli anapaswa kuondolewa kwenye lawama, na zibaki kwa Mbowe. Na swali ni nafasi gani mgombea urais aliichezea? Mgombea Urais Chadema 2020 alikuwa Lissu. Hivyo, kwa nadharia ya Coattail Effect, Lissu kutokuwezesha Chadema kupata wabunge wengi, maana yake hakuwa na mvuto.

Je, wa kulaumiwa ni Mbowe au Lissu ambaye ndiye aliyebeba bendera ya chama? Wakati wa Uchaguzi Mkuu, nyota wa chama ni mgombea urais. Ushawishi wake hujenga, huimarisha au kubomoa chama. Ipi nafasi ya Lissu ikiwa Mbowe atalaumiwa? Utaona kuwa maneno ya kampeni yanadhoofisha zaidi Chadema. Yanaitetea na kuisafisha CCM.

Related Posts