Tanzania ilivyojipanga mashindano ya Chan

Kamati ya ndani ya Tanzania ya maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan) 2025 imesema kuwa Tanzania iko tayari kuandaa fainali hizo mwezi ujao.

Fainali hizo zitafanyika kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28 mwaka huu katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zikishirikisha mataifa 19.

Mwenyekiti wa kamati ya ndani ya maandalizi ya Chan 2025, Leodegar Tenga alisema juhudi kubwa zimefanyika kuhakikisha maandalizi hayo yanakwenda kama yalivyopangwa na kwa sasa nchi iko tayari kwa mashindano hayo.

“Ili kufanikisha mashindano hayo, Serikali imefanya maandalizi muhimu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano hayo ambao umefanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa na Uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar.

“Vilevile kwa matakwa ya CAF vimejengwa viwanja vya mazoezi vya Gymkhana, Law School na Meja Jenerali Isamuhyo ambavyo vitatumika kwenye mashindano ya CHAN.

“Maandalizi haya ya miundombinu hii ya yamefikia asilimia zaidi ya tisini na tano. Aidha, ili kujiridhisha na maandalizi yanayofanyika Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (Caf) limekuwa likifanya ukaguzi wa mara kwa mara na wameridhishwa na maandalizi pamoja na utayari wa nchi yetu kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ingawa kuna mambo kadhaa tunaendelea kuyakamilisha,” alisema Tenga.

Tenga alisema kuwa kuanzia sasa, Watanzania wanapaswa kukaa mkao wa kula na kuwa tayari kuchangamkia fursa za Chan.

“Katika muendelezo wa maandalizi haya hususan kwa upande wa hamasa,  limeandaliwa kongamano kubwa la wadau wa michezo litakalofanyika kesho tarehe 15/01/2025 katika Ukumbi wa Johari Rotana kuanzia saa tatu kamili asubuhi. Lengo la kongamano hilo ni kutoa taarifa kwa wadau kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Chan.

“Tuna uhakika kwamba timu mwenyeji itachezea kwao. Chan ni shindano la watoto wetu. Wachezaji wa ndani, tuwape hamasa,” alisema Tenga.

Related Posts