Singida Black Stars yafuata mido Burkina Faso

SINGIDA Black Stars imetua kambi ya timu ya Taifa ya Burkina Faso ikipambana kuipata saini ya Clement Pitroipa mwenye uwezo wa kucheza kiungo mshambuliaji na ukabaji.

Pitroipa alikuwa nyota wa mchezo wakati Burkina Faso ikiichapa Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika juzi Jumatatu Kisiwani Pemba akifunga bao moja na kutengeneza lingine wakishinda 2-0.

Taarifa za ndani kutoka Singida Black Stars ni bosi mmoja wa juu wa timu hiyo ametuma mwakilishi wake kwenda kuteta na Pitroipa.

Pitroipa hana shida kumalizana na Singida, lakini ametaka mabosi wa matajiri hao wa Singida Black Stars kuwasiliana na klabu yake AS Douanes ya kwao Burkina Faso.

Hata hivyo, Singida Black Stars itahitajika kufanya kazi ya ziada kuvunja mkataba wa kiungo huyo uliobaki mwaka mmoja na nusu ndani ya klabu yake ya AS Douanes.

Endapo Singida Black Stars ikikamilisha usajili wa kiungo huyo kabla ya leo dirisha halijafungwa, basi italazimika kupunguza mtu ili kuchukua nafasi yake.

Kwa sasa timu hiyo ina wachezaji 14 wa kigeni na kanuni zinaruhusu wawepo 12 kwa kila timu hivyo tayari imezidisha wawili.

Wachezaji hao ni Jonathan Souwah, Morice Chukwu, Emmanuel Lobota, Victorien Adebayor, Abdolaye Camara, Elvis Rupia, Marouf Tchakei, Mohamed Damaro, Josephat Bada, Emmanuel Keyekeh, Ibrahim Imoro, Anthony Trabi Tra, John Nekadio na Frank Assinki.

Related Posts