Moto unavyozidi kuitesa Marekani, vifo vyafikia 25

Los Angeles. Idadi ya waliofariki kutokana na moto unaoendelea kuteketeza makazi ya watu na maeneo mbalimbali jijini Los Angeles Marekani imeongezeka na kufika watu 25.

Taarifa ya kuongezeka kwa vifo hivyo imetolewa alfajiri ya kuamkia leo Jumatano Januari 15, 2025, na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Jimbo la Los Angeles huku ikisema idadi hiyo huenda ikaongezeka kutokana na idadi ya watu wanaokadiriwa 13 hawajulikana walipo.

Tovuti ya CNN, imeripoti kuwa Naibu Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto eneo la Los Angeles, Brice Bennet, ametoa taarifa kwa umma kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) akisema kuwa maeneo yanayozunguka milima ya San Luis Obispo na Santa Barbara yatawekewa bendera nyekundu kuashiria kuwa yako hatarini kufikiwa na moto huo.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa limetoa tahadhari ya hatari inayoweza kutokea wakati wowote kuhusiana na moto huu.

“Kuna upepo mkali unaovuma kwa kasi ya kati ya kilometa 55 hadi 70 kwa maeneo mengi Jumatano ya leo. Tayari upepo huo umeanza kupuliza na unatarajiwa kuwa hatari zaidi ikifika jioni,” amesema Bennet.

“Upepo huu unatarajiwa kuwa hatari kwa sababu utakuwa unasambaza moto, katika maeneo mengi hususani ni maeneo ambayo hatujaweza kuyafikia,” ametahadharisha Bennet.

Amesema takriban makazi 90,000 eneo la Los Angeles hayana huduma za msingi ikiwemo umeme baada ya huduma hizo kukatwa kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa moto huo.

Hadi kufikia Jana jioni, Bennet amesema maeneo yaliyokuwa hatarini zaidi kukumbwa na moto huo jijini Los Angeles ni pamoja na yenye maelfu ya wakazi hususan ni Oaks, Northridge na Simi Valley, ambako ni nyumbani kwa wakazi zaidi ya 300,000.

Mamlaka jijini humo zimeamuru wananchi kuvaa barakoa kwa kile kinachotajwa ni upepo mkali unaopuliza kuwa unaweza kusababisha kusambaa kwa hewa ambayo huenda ikawa na vimelea wa magonjwa.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Jimbo la Los Angeles, Anish Mahajan, majivu yanayopulizwa kutoka maeneo ya makazi na misitu iliyoteketezwa eneo la Palisades linaweza kusababisha madhara kwa binadamu.

“Upepo mkali unaweza kuchangia kusambaza kwa kupuliza vumbi kwa wingi kutoka Mashariki mwa Palisades na maeneo mengine ambayo kuna magari yaliyoteketea katika moto huo,” amesema Mahajan.

 “Upepo unaopuliza majivu unaweza kuwa unajumuisha kemikali zilizotokana na vitu vilivyoteketea, yatupasa kuchukua tahadhari wakati wote dhidi ya magonjwa,” amesema.

Mahajan amewataka wananchi na wakazi wa eneo hilo kuvaa barakoa aina ya N95 ama P100 wakati wote iwapo watakuwa katika maeneo yaliyoathiriwa na moto huo.

Takwimu zinaonyesha takriban maofisa 1,850 wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo, wamesambazwa na wameungana na maofisa wa zimamoto wa Marekani, Canada na Mexico kupambana na moto huo.

Kati yao, mamia ya wanajeshi hao kutoka California, Nevada na Wyoming wanapambana kuuuzima kwa kutumia ndege wakati huu ambao moto huo unatajwa kubadilisha uelekeo kila mara kutokana na upepo huo.

 “Tunatoa pole sana kwa familia za walioathiriwa na moto huu hususan ni eneo la Los Angeles,” amesema Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo, Jenerali Steve Nordhaus.

 “Kusaidia jamii hususan zenye uhitaji ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya Jeshi letu. Na tunajivunia watu wote wanaume kwa wanawake ambao wanafanya kila liwezekano kuhakikisha wanaudhibiti moto huu kutoka katika vikosi vya kupambana na majanga na mataifa ambayo ni marafiki zetu,” amesema.

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Polisi Los Angeles, Jim McDonnell amesema: “Wakati huu ambao tunaingia kwenye kipindi chenye upepo mkali, tutaendelea kufanya kazi eneo lenye moto huu wakati wote tayari kukabiliana nao na kuwaondoa wananchi ambao maeneo yao yamesogelewa na moto hu.”

Ameongeza kwa kuwataka wananchi wa eneo ulipofika moto huo kufuata maelekezo wanayopewa ikiwemo kuondoka wanapohitajika kufanya hivyo ili kuepuka madhara ikiwemo kujeruhiwa ama kufariki kutokana na moto huo.

Ofisa huyo pia amesema watu 39 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kukiuka masharti yaliyotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama jijini humo ikiwemo kuingia kwenye makazi ya waathiriwa na kuiba mali.

“Tunachoweza kuwahakikisha ni kwamba Polisi jijini Los Angeles tumejipanga kukabiliana na kila mwenye nia ya kutumia janga hili kujinufaisha,” amesema.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts