Seoul. Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk-Yeol amekamatwa nyumbani kwake jijini Seoul nchini humo.
Al Jazeera imeripoti leo kuwa Rais Yoon, ametiwa nguvuni leo Jumatano Januari 15, 2025, baada ya maelfu ya askari kutoka Idara ya Kupambana na Rushwa (CIO) na Polisi nchini humo kufurika nyumbani kwake.
Misururu ya magari ya askari hao aina ya SVU na mengine yakiwa na ving’ora yameonekana yakiondoka katika makazi ya Rais Yoon huku yakisiindikizwa na magari ya Jeshi la Polisi nchini humo.
Kukamatwa kwa Rais Yoon, ni jaribio la pili katika kipindi cha wiki mbili lililozaa matunda tangu Mahakama ya Katiba nchini humo itoe amri Rais huyo akamatwe kujibu tuhuma kuhusiana na uamuzi wake wa kutangaza nchi hiyo kuongozwa chini ya Sheria ya Kijeshi (Martial Law).
Kabla ya kukamatwa kwake, maofisa wa Juu wa CIO walionekana wakizungumza na wanasheria wa Rais Yoon ndani ya makazi yake huku maelfu ya waandamanaji wanaomuunga na wasiyomuunga mkono Rais huyo wakishuhudia.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Rais huyo, Rais Yoon amekubali kufanyiwa uchunguzi kuhusiana na madai ya rushwa na uhaini yanayomkabili.
Amesema Rais Yoon alikuwa tayari kutoa ushirikiano na kwenda zilipo ofisi za Makao Makuu ya CIO jijini Gwacheon, pindi maofisa hao na polisi watakapoondoka katika makazi yake.
Hata hivyo, suala la Rais huyo kujipeleka mwenyewe halikukubalika hadi pale maofisa hao walipovamia makazi yake na kumchukua kimabavu kisha kuondoka naye.
Hata hivyo dalili hazionyeshi kuwa maofisa waliomkamata wamekumbana na upinzani mkubwa, kwa kile kinachodaiwa kuwa wakati wanaingia katika makazi hayo hawakukumbana na upinzani wowote.
Yoon alitangaza Korea Kusini kuwa chini ya Sheria ya Kijeshi Desemba 3, 2024, kwa alichodai ni uamuzi unaolenga kulinda uhuru wa taifa hilo dhidi ya uvamizi wa mataifa ya nje jambo ambalo lilipingwa vikali na wabunge wa upinzani na kuzuia maandamano ya raia mitaani kuupinga.
Ofisi ya Idara ya kupambana na Rushwa ndiyo inaongoza japo la maofisa na vikosi vya kijeshi vinavyofanya uchunguzi dhidi ya uamuzi wa Rais huyo unaohusishwa na uhaini, makosa ambayo yanaweza kusababisha ahukumiwe kifungo cha maisha jela ama hukumu ya kifo.
Jitihada za kumkamata zilianza Januari 3, mwaka huu, hata hivyo ziligonga mwamba baada ya maofisa na walinzi wa Rais huyo kuzuia jaribio la kukamatwa kwake.
Baada ya saa kadhaa za kusimama nje ya makazi ya rais huyo, maofisa wa Idara ya kupambana na Rushwa nchini humo, wachunguzi na polisi walionekana wakipandisha kuelekea lilipo geti la nyumba ya Rais huyo.
Maofisa wa polisi walionekana mwanzo wakitumia ngazi kupanda juu ya ukuta kwa kutumia mabasi yao kuangalia hali ya usalama ndani ya jengo hilo.
Maofisa wengine walionekana wakiingia ndani ya makazi hayo kwa kutumia mlango wa usalama uliopo pembeni ya geti la jengo hilo baadae walionekana wakizungumza na mmoja wa mwanasheria wa Rais Yoon.
Baada ya muda kupita, walinzi wa Rais huyo walionekana wakiondoa magari yaliyokuwa yameegeshwa njiani kuzuia maofisa hao wasiingie ndani ya nyumba na kumkamata Rais huyo.
Seok Dong-hyeon, ambaye ni Mwanasheria wa Rais Yoon, amesema wanasheria wake walikuwa wakizungumza na maofisa hao juu ya kumruhusu ajisalimishe mwenyewe kwa mahojiano.
Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa baada ya maofisa waliofika kumkamata kudai wanatakiwa kutekeleza amri ya Mahakama ya kumchukua na kumfikisha katika ofisi yao kwa mahojiano muda mfupi baada ya kufanikiwa kupenya katika makazi yake yaliyozungushiwa uzio wenye nyaya za Umeme.
Baada ya kufanikiwa kumkamata Rais Yoon, CIO na vitengo vingine vya usalama vitatakiwa kuomba kibali cha Mahakama ili kuendelea kumshikilia, la sivyo, Rais huyo ataachiwa ndani ya Saa 48 kwa mujibu wa Sheria za nchi hiyo.
Baada ya kukamatwa, Rais Yoon alisikika akisema amekubali kukamatwa na maofisa hao, huku akiuita ukamataji huo dhidi yake kuwa unakiuka sheria na miongozo ya nchi hiyo.
“Niliamua kwenda ofisi za CIO, japo uchunguzi batili unaofanyika. Kwa lengo la kuzuia umwagikaji damu wowote ule ninakubali kukamatwa,” alisikika akisema Rais Yoon.
“Pamoja kukubali kukamatwa ila haimaanishi kuwa nakubaliana na uchunguzi wao dhid yangu,” amesema Rais huyo.
Katika kipande hicho cha video, Rais Yoon anasikika akisema utawala wa sheria nchini Korea Kusini umevunjwa na Ofisi za Serikali zinazomchunguza na Mahakama inayosikiliza shauri lake kwa kile anachodai hazina mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
Amemalizia kwa kusema kuwa pamoja na kuwa anapitia siku nyeusi, ila anaamini kesho yake itakuwa ya matumaini.
“Ujumbe wangu kwa wananchi wangu nawatakia kila la Heri nawaomba muwe imara na Asanteni sana,” amesema Rais huyo.
Hatima yake imesalia mikononi mwa Mahakama ya Katiba, ambayo ilianza jana usikizaji wa shauri linalomkabili na itaamua iwapo uamuzi wa kutangaza nchi hiyo kuoingozwa kijeshi ulipaswa kufanyika ama ni uhaini.
Ikibainika haukuwa halali, Rais Yoon anaweza kutiwa hatiani na kupewa adhabu ya kifungu cha maisha jela ama hukumu ya kifo.
Usikizwaji wa kesi yake itaendelea tena kesho Alhamisi baada ya jana kesi yake kusikilizwa kwa dakika tano pekee kisha kupigwa kalenda baada ya Rais huyo kutokuwepo mahakamani.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa Msaada wa Mashirika.