NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameeleza kusikitishwa na kitendo cha Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilayani humo kushindwa kushirikisha jamii husika kwenye maeneo mbalimbali ambako kunatekelezwa miradi ya maji hali inayopelekea kutokea malalamiko kutokana na kutoelewa nini kinaendelea.
Kasilda ameeleza hayo baada ya malalamiko ya wakazi wa Kijiji cha Bangalala kwenye mkutano wa hadhara wakidai kusitishiwa huduma ya maji kwenye jumuiya ya watumia maji Mhetute takribani miezi mitatu pasipo kupatiwa taarifa yeyote kutoka kwa mamlaka husika.
“Waziri wa Maji Jumaa Aweso yupo vizuri sana lakini tukija huku chini mnamuangusha sana, yani lazima mbadilike RUWASA haiwezekani ulete mradi kwenye Kijiji halafu wananchi wa eneo husika hawajui chochote kuhusu huo mradi”. Alisema Kasilda.
Aidha amemuagiza Afisa Tarafa ya Mwembe Mbaga, kuitisha mkutano wa hadhara ndani ya wiki moja kutekeleza takwa la kisheria kuchagua viongozi watakao simamia mradi huo kuwa na matumizi endelevu, ambapo pia husaidia kudhibiti kuhujumiwa kwa miradi inayotekelezwa kwani wananchi watakuwa na ufahamu juu ya utekelezaji wake.